MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mama Mariam Mwinyi ameushukuru uongozi wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar kwa kukubali kupokea sadaka ya Iftar na kutaka itumike vyema kama ilivyokusudiwa.Akizungumza na Uongozi wa Chuo cha Mafunzo katika makabidhiano ya sadaka hiyo yaliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo hicho Kilimani Jijini Zanzibar,kwa niaba ya Mama Mariamu Mwinyi, Mjumbe wa Bodi ya Jumuiya ya Maisha Bora Foundation Jaha Haji Khamis alisema sadaka hiyo inapaswa kutumika, walengwa wakiwa ni wanafunzi wa kike wa chuo hicho.

Alisema utoaji wa sadaka hiyo ni hatua ya utekelezaji wa azma ya Jumuiya ya kuhakikisha inatoa msukuimo katika kunyanyua maisha ya vijana na wanawake.

Nae, Mkuu wa Utawala wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar Mrakibu Omar Hamduni Mjomba aliishukuru Jumuiya hiyo chini ya Mwenyekiti wake Mama Mariamu kwa kuona umuhimu wa kukabidhi msaada huo.“Kutoa ni moyo, zipo taasisi nyingi zenye uwezzo mkubwa tu na hazijafanya hivyo”, alisema.

Alisema msaada huo umekuja kwa wakati muafaka na hivyo akachukua fursa hiyo kuutaka uongozi wa Gereza kuhakikisha unatumika vyema ili kuwasaidia wanaafunzi wa kike walioko Gerezani katika kipindi hiki mwezi mtukufu wa Ramadhani na sikukuu ya ya Idd el Fitr.Aidha, aliiomba Jumuiya hiyo kufikiria uwezekano wa kutoa misaada kama hiyo kwa wanafunzi wa jinsia ya kiume, pale hali itakaporuhusu.

Miongoni mwa sadaka ya Iftari iliokabidhiwa na Jumuiya hiyo ni pamoja na Mchele, Tende, mafuta ya kupikia, maharage pamoja na chumvi.