MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mama Mariamu Mwinyi amesema kilimo cha zao la Mwani kina manufaa makubwa kwa Afya na Uchumi wa Wazanzibari.Mama Mariamu amesema hayo Ikulu ndogo Migombani, alipozungumza na Ujumbe wa Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika Mataifa mbali mbali Duniani, ambapo pamoja na mambo mengine aliwaelezea juu shughuli mbali mbali zinazofanywa na Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), sambamba   na utekelezaji wa Programu ya miaka mitatu ya taasisi hiyo.

Amesema wastani wa asilimia themanini (80%) ya wakuliwa wa kilimo wa zao hilo ni wanawake, huku akibainisha malengo ya kuliongezea thamani zao hilo ili kuleta tija kwa wakulima na Taifa kwa ujumla.Aidha, mama Mariamu aliwafahamisha Mabalozi hao changamoto mbali mbali zinazowakabili walengwa wa Programu hizo (wanawake, vijana na watoto), ikiwemo vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia pamoja na azma ya kuwapatia taulo za kike wanafunzi wa kike walioko shuleni.

Amesema pamoja na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali katika kukabiliana an vitendo vya udhalilishaji, bado hali sio nzuri, akibainisha kuwepo wimbi kubwa la vitendo hivyo hapa nchini, huku tatizo hilo likichangiwa kw akiasi kikubwa na jamii (waathirika) kutokana na aibu pamoja na muhali.Aidha, amesema kumekuwa na juhudi za kuimarisha afya za vijana kwa kufanya mazoezi, lengo likiwa ni kuhakikisha Taifa linakuwa na wananchi wenye uwezo wa kufanya kazi.
Mama Mariamu alieleza kuwa ZMBF imekuwa katika juhudi za kukabiliana na Vifo vya mama na watoto kupitia Programu yenye lengo la kuielimisha jamii umuhimu wa Lishe bora kwa watoto.

Alisema malengo yamelekezwa kwa watoto hususan walio chini ya umri wa miaka mitano, huku mkazo ukiwekwa katika uimarishaji wa afya ya mama kabla ya uzazi .

Nae, Kiongozi wa Mabalozi hao Asha Rose Migoro alipongeza juhudi zinazochukuliwa na taaasisi hiyo ya ZMBF na kuahidi kushirikiana an washirika wa Maendeleo katika nchi wanazofanyia kazi, ili kufanikisha malengo ya Taasisi.Amesema takriban nchi zote zenye uwakilishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zimeweka vipaumbele katika ushughulikiaji wa masuala ambayo ZMBF imelenga kuyatekeleza.