MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mama Mariamu Mwinyi amesisitiza umuhimu wa akinamama wa kiislamu nchini kuwatii waume zao pamoja na kutekeleza haki zao katika mambo yalioelekezwa na Mwenyezi Mungu.
.
Mama Mariamu ameeleza hayo katika nasaha alizotowa kwa akinamama wa kislamu walioshiriki katika Maulid ya kumswalia Mtume Muhammad (SAW) yaliofanyika katika Msikiti wa Muembeshauri, Mkoa Mjini Magharibi.

Maulid hayo yameaandaliwa na Jumuiya ya akinamama wa Msikiti wa Mwembeshauri, ambapo yamewashirikisha waislamu kutoka maeneo mbali mbali ya Zanzibar na Tanzania Bara.

Amesema kuna umuhimu mkubwa kwa akinamama wa kislamu kuwatii waume zao katika kutekeleza mambo mema, na akatumia fursa hiyo kumuomba Mweneyzi Mungu kuizidishia utiifu jamii hiyo.

Aidha,Mama Mariamu alikubali maombi ya kuwa Mlezi wa Jumuiya hiyo pamoja na kusaidia harakati za kuiendeleza katika kufanikisha ujenzi wa jengo lake, sambamba na msada wa huduma za kujikumu kwa wageni waliotoka Mtwara Tanzania Bara, ambao watakuwepo zanzibar kw akipindi cha wiki moja.

Nae, Makamo Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Fatma Mliwa akitoa mawaidha katika Maulid hayo alisema uzawa wa Mtume Muhammad (saw) ni fadhila na rehemu kubwa kutoka Mwenyezi Mungu, kwani amekuja kubainisha mazuri na mabaya.

Aidha, Bi Ashura kutoka Mtwara akitowa salamu za akinama kutoka Mtwara aliishukuru Jumjuiya hiyo ya akinamama w aMsikiti wa Muembe Sahuri kwa mwaliko walioupata na katumia fursa hiyo kuondosha dhana kuwa Maulid ni Bidaa na hivyo akasisitiza umuhimu wa kumsifia Mtume.

Mapema, akitoa mawaidha katika maulid hayo Bi Mkubwa Omar alisitiza umuhimu wa akinamama wa kiislamu kuwatii na kutekeleza haki za waume zao, huku akibainisha mambo mbali mbali wanayopaswa kutekeleza ikiwemo la kutotoka nyumbani bila ridhaa za waume zao pamoja na kudai talaka bila sababu zozote za msingi.