Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema ili nchi za Kiafrika ziweze kutekeleza vyema mageuzi ya kiuchumi na kukuza ustawi wa wananchi, ni lazima kuwa na sekta na taasisi za Bima zilizo imara na zenye kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya Sayansi na Teknolojia katika karne ya 21.

Dk.Mwinyi amesema hayo katika ufunguzi wa Mkutano wa Bima kwa nchi za Afrika, uliofanyika katika Hoteli ya Madinat Bahr, ulioko Mbweni Jijini Zanzibar.Amesema katika kujenga na kuendeleeza uchumi wa kisasa, uwepo wa mfumo, sheria na taratibu madhubuti za uendeshaji wa shughuli za Bima ni muhimu ili kuwapa wawekezaji imani na uhakika wa usalama wa mitaji wanayotaka kuwekeza.

Alisema pamoja na kuwepo maendeleo katika sekta hiyo,  Afrika inapaswa kuendelea kuimarisha sekta hiyo ili iweze kuyafikia makundi yote ya wannachi yanayojishughulisha na shughuli mbali mbali za kiuchumi,  hususan katika sehemu za vijijini.Alisema wananchi wengi wamekuwa wakiendesha shughuli zao bila ya kuwa na kinga ya Bima, hivyo akatumia fursa hiyo kutoa wito kwa Mataifa ya Afrika kuwaelimisha wananachi wao umuhimu wa kuwa na Bima,pamoja na kutaka Bima hizo zitolewe kwa gharama nafuu na kwa wakati muafaka, hususan pale wananchi wanapopata misukosuko ya kiuchumi.

Rais Dk. Mwinyi akaelezea furaha aliyonayo kutokana na maudhui ya mkutano huo yanayosisitiza umuhimu wa kuongeza juhudi katika kufikisha huduma za Bima kwa wananchi wengi zaidi ili kukuza sekta hiyo, ikiwemo Bima ya Afya, Bima ya Maisha, pamoja na kuwajengea uwezo watendaji.Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalenga kuanzisha Bima ya Afya, ikiwa ni hatua ya kuimarisha utoaji wa huduma hizo kwa wananchi, ambapo kwa kipindi kirefu ilishindwa kukidhi haja kutokana na kutegemea Bajeti yake kwa asilimia mia moja.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuzialika Kampuni mbali mbali za Bima Barani Afrika kuja kuwekeza Zanzibar ili kuendeleza uchumi wa Buluu, akibainisha kuwepo fursa nyingi za kiuchumi .

“Hatutopenda Wawekezaji tunaowavutia kuja kuwekeza Zanzibar kwenye Bandari za kisasa, kwenye uvuvi, kwenye mafuta na Gesi,  wanakata Bima zao nje,  ni vyema tukahakikisha Bima zao wanakata hapa hapa nchini”, alisema.

Dk. Mwinyi aliwahakikishia washiriki wa mkutano huo, kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Kampuni mbali mbali za Bima Barani Afrika, ili kuhakikisha malengo ya kufikisha huduma bora za Bima kwa wananchi wote Mjini na Vijijini zinafikiwa.

Nae, Waziri wa Nchi (OR) Fedha na Mipango Jamal Kassim Ali alisema ni wakati muafaka kwa washiriki wa mkutano huo kujadili umuhimu wa shughuli za Bima ya Afya Barani humu, kuambatana na Azimio la Abuja (Abuja Declaration).

Aidha, Katibu Mkuu Wizara ya Nchi, (OR) Fedha na Mipango Dk. Malik Akil alisema Serikali inaamini kuna kazi kubwa inayopaswa kufanyika ili kuhami rasilimali za Bahari na zile zenye mnasaba na hizo ili kuiwezesha Zanzibar kufikia azma ya kuimarisha uchumi wa Buluu.

Mapema, Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Khadija Issa Said alisema pamoja na mafanikio makubwa yaliopatikana katika uendeshaji wa Sekta ya Bima Afrika na hususan Tanzania, kuna changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta hiyo, ikiwemo uelewe mdogo wa wananchi, hususan walio vijijini.