RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la   Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Mwinyi amewataka waumini wa Dini ya Kiislamu kuitumia Misikiti kwa ajili ya kupata elimu itakayowawezesha kutekeleza vyema ibada zao.Alhaj Mwinyi ametoa wito huo katika ufunguzi wa Msikiti wa Mohamed Bin Ahmeid bin Al-Jofair uliopo Chuini Wilaya Magharibi ‘A’ Unguja katika hafla iliokwenda sambamba na Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Amesema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa msikiti huo, waislamu wana wajibu wa kuwa na Madrasa itakayowawezesha waumini kupata elimu ya dini na kufanya ibada kwa usahihi.Alhaj Dk. Mwinyi aliahidi kuchangia ununuzi wa upatikanaji wa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Madrasa hiyo.

Aidha, aliwataka waumini kuutendea haki msikiti huo kwa kushiriki kwa wingi katika ibada na kuondokana na utamaduni wa kusubiri hadi za siku za Ijumaa au mfungo wa mwezi wa Ramadhani.Alhaj Mwinyi aliwashauri waumini wa msikiti huo kuwa na utaratibu utakaowawezesha kupata mapato kwa ajili ya matunzo ya msikiti pamoja na kuwasaidia masheikh na maimamu wanaowaongoza.

Alitumia fursa hiyo kuwataka waislamu kuutunza msikiti huo ili uendelee kuwa bora na wenye kupendeza kwa kipindi kirefu kijacho.

Vile vile aliwatakia kheri na malipo mema wafadhili pamoja na waumini wote waliojitolea kwa hali na mali katika kufanikisha ujenzi wa msikiti huo.

Nae, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Omar Saleh Kaab aliwataka waumini wa msikiti huo kuutumia kikamilifu kwa ajili ya kumtii Mwenyezi Mungu pamoja na kujikita katika ibada.


Katika hatua nyengine , Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Mufti wa Zanzibar Skekh Khalid Ali Mfaume alisitiza umuhimu wa waislamu kuimarisha misikiti kwa kufanya usafi ili kuiwezesha kubaki katika ubora wake na akabainisha hatua hiyo kuwa na malipo makubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Aidha, aliwataka kuutumia msikiti huo kwa ajili ya kupata elimu sambamba na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazoikabili jamii, ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya.

Mapema, Khatibu wa Sala hiyo ya Ijumaa Sheikh Rashid Salim alisema misikiti ipo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, hivyo akawakumbusha waislamu jukumu la kuutumia vyema kwa ibada na kuepuka vitendo vyote vya kumshirikisha Mwenyezi Mungu.

Aliwataka kuendelea kushikamana na kuepuka mifarakano na kusema Mwenyezi Mungu anachukia ‘usengenyi’ kwa kigezo kuw husabaisha ugonvi na mifarakano.

Aliwataka waumini kuondokana na vitendo vya kusengenya , akibainisha watu wanaofanya vitendo hivyo watarejea kwa Mola wao il-hali wakiwa wamefilisika.

Aidha, alikemea na kuwataka waumini kuondokana na uharibifu wa mali pamoja na udadisi unaojenga dhana. 

Alitumia fursa hiyo kuwashukuru wafadhili pamoja na waumini walioshiriki kwa namna tofauti kufanikisha ujenzi wa msikiti huo.

Msikiti huo wa Mohamed Bin Ahmeid Bin Al-Jofair wenye uwezo wa kuswaliwa na waumini 600 kwa wakati mmoja,  ujenzi wake ulianza mnamo mwaka 2018 kupitia kwa wafadhili na kugharimu kiasi cha shilingi Milioni 160 hadi kukamilika kwake.