Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini mchango wa Jumuiya ya Magoa Zanzibar katika kuendeleza shughuli za maendeleo zikiwemo huduma za kijamii.Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Jumuiya ya Magoa Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Bi Amanda Demello.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Jumuiya ya Magoa Zanzibar kama zilivyo jumuiya nyengine imekuwa na mchango mkubwa katika kuiunga mkono Serikali kupitia shughuli mbali mbali za maendeleo zikiwemo za biashara, huduma za kijamii, uwekezaji na hata sekta ya utalii.Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Jumuiya hiyo katika kuhakikisha inatekeleza vyema shughuli zake zikiwemo huduma zake za kiroho kwa azma ile ile ya kuendeleza amani na utulivu.

Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba ni jukumu la Serikal katika kuwapelekea wananchi huduma muhimu za kijamii lakini kutokana na uwezo wake kuwa mdogo Jumuiya kama hizo zimekuwa zikiiunga mkono Serikali kutoa huduma hizo kwa wananchi jambo ambalo ni la msingi na la kupongezwa.Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba ujio wa Jumuiya hiyo Ikulu na kupata fursa ya kuzungumza mambo mbali mbali ikiwa ni pamoja na kueleza changamoto walizonazo kuna zidi kuleta uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Serikali na Jumuiya hiyo.

Akizungumzia juu ya suala la uwepo wa mapapasi ambao wamekuwa wakiwasumbua wageni wanaotembelea Mji Mkongwe pamoja na fungwe mbali mbali katika visiwa vya Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba juhudi za makusudi zitachukuliwa kupitia kikosi maalum cha askari wa Utalii katika kuhakikisha mambo kama hayo hayatokea kwani yanaitia dosari sekta hiyo hapa nchini.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alitilia mkazo suala la kupewa kipaumbele kwa somo la Historia katika skuli za Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba sekta ya utalii ambayo ndio sekta muhimu katika uchumi wa Zanzibar inahitaji historia hasa kwa utalii wa Zanzibar ukiwemo Mji Mkongwe.Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kueleza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuupitia upya mfumo mzima wa elimu ya Zanzibar ili iweze kuleta mabadiliko makubwa na kurudi katika hadhi yake kama ilivyokuwa hapo kabla.

Mapema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Magoa Zanzibar, Bi Amanda Demello alitoa shukurani kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kuipa Jumuiya hiyo fursa ya kukutana nae na kuweza kubadilishana nae mawazo.

Akieleza historia fupi Bi Amanda alieleza kwamba Magoa walianza kuingia Zanzibar mnamo karne ya 18 kutoka Goa, nchini India kwa kutumia majahazi na meli za abiria.Aliongeza kuwa katika karne ya 20 Magoa waliongezeka na kuwa wengi zaidi katika visiwa vya Zanzibar, Unguja na Pemba na kushika nyadhifa mbali mbali ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kabla ya Mapinduzi na baada ya Mapinduzi

Katika maelezo yake Bi Amanda alitumia fursa hiyo kueleza changamoto inazoikabili Jumuiya yao ikiwa ni pamoja na kukosa sehemu ya kukutana pamoja na kufanya shughuli zao kama ilivyo kwa jumuiya kama hiyo kwa upande wa Dar-es-Salaam, Arusha, Nairobi, Tanga na Mombasa.

Hivyo, Mwenyekiti huyo alieleza kwamba Jumuiya ya Magoa walioko Zanzibar ina matumaini makubwa na Serikali anayoiongoza Rais Dk. Mwinyi kwani wanakubaliana na maendeleo yaliyofanyika kwa muda mfupi aliokaa madarakani na wanazikubali juhudi anazozichukua za kimaendeleo na kuwaweka wananchi wote wa Zanzibar kuwa kitu kimoja.

Nae Bwana Wolfango Bosco Martins (Bulu), alitumia fursa hiyo kutoa historia ya Magoa hapa Zanzibar pamoja na shughuli mbali mbali wanazozifanya na zile ambazo waliwai kuzifanya wao na wazee wao zikiwemo za utumishi Serikalini