RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amepokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Ikulu, Zanzibar.Akipokea ripoti hiyo Rais Dk. Mwinyi amemuomba Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora kuiwasilisha katika Baraza la Wawakilishi.

Akizungumza baada ya kukabidhi riporti hiyo kwa Rais Dk. Mwinyi, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Dk. Othman Abass Ali CAG, alisema wamewasilisha ripoti saba ikiwemo ya Serikali Kuu (Mawizara na taasisi zote), Mashirika na Taasisi zinazojitegemea, ripoti ya Idara Maalum na taasisi zake, ripoti ya mifumo yote ya Tehema ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ripoti ya mashirika ya Umma, na ripoti ya ufanisi ya miradi ya Maendeleo iliyofadhiliwa na fedha za Uviko 19.

Alisema ripoti hizo zipo za aina mbili ikiwemo miradi ya maendeleo ya wahisani pamoja na ya Serikali pamoja na ripoti za kiufundi.“Tunapojenga tunatakiwa kufanya ukaguzi wa thamani ye fedha, tumefanya ukaguzi huu kwa sekta za Afya na Elimu kwa skuli zote 12 zilizojengwa” alielza CAG.Pia alieleza walifanya ukaguzi kwa skuli ya Bweleo ambayo Serikali iliinunua na skuli zote zilizofanyiwa matengenezo ikiwemo vyoo vya skuli hizo na kuonesha yote yaliyobainika kwenye ukaguzi huo.

Kifungu cha 112 (5) kinamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali awasilishe taarifa yote aliyoikagua na aikabidhi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa hatua nyengine.