RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema atahakikisha mapendekezo yaliowasishwa kwake na Kamati maalum aliyounda kuchambua maona mahsusi ya Wazanzibari yanafanyiwa kazi kikamilifu.Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Zanzibar katika hafla ya makabidhiano ya Ripoti maalum iliochambua maoni mahsusi ya Wazanzibar kuhusiana na mustakbali mwema wa kisiasa hapa nchini.
Alisema akiwa kiongozi wa nchi atahakikisha mapendekezo yaliowasishwa kwake yanafanyiwa kazi kikamilifu hatua kwa hatua baada ya kupata ushauri kutoka kwa wataalamu kwa kuzingatia baadhi ya mapendekezo hayo yanagusa moja kwa moja Katiba ya Zanzibar.“Ripoti itawasilishwa kwa wataalamu ili washauri namna ya utekelezzaji wake kwa kutambua kuwa baadhi ya mapendekezo yapo yanayohusu Katiba”, alisema.
Alisema lengo kuu ya kuundwa kwa kamati hiyo ni kuendeleeza amani iliopo hapa nchini, kujenga umoja pamoja na kutafuta njia za kuendeleza maridhiano yaliofikiwa.Alisema Zanzibar haiwezi kukuza uchumi wake bila ya kuwepo umoja na amani nchini.
Dk. Mwinyi alisema ni jambo la faraja kuwa kazi hiyo imefanywa na Wazanzibari wenyewe kwa ufanisi mkubwa na akatumia fursa hiyo kuwapongeza wajumbe wa Kamati hiyo kwa kufanya kazi nzuri na kuikamilisha kwa wakati.
Aidha, alisema alitambua kuwa mijadala ndani ya kamati hiyo itakuwa mizito, lakini akabainisha furaha yake kwa wajumbe wa kamati hiyo kufikia makubaliano na kila mjumbe kuweza kusaini ikiwa ni hatua ya kuridhika na yale yaliofikiwa.
Mapema, Mwenyekiti wa Kamati maalum ilioratibu maoni mahsusi ya Wazanzibar katika mustakbali wa kisiasa nchini, Dk. Ali Ahmeid Uki akiwasilisha Ripoti hiyo alisema Kamati hiyo imetekeleza majukumu yake katika kipindi cha siku 15 na kufanikiwa kutoa mapendekezo kadhaa pamoja na ushauri.Alisema ripti hiyo imejumuisha mambo kadhaa yaliojadiliwa ambayo yamegawanywa katikka sura kuu nne, na akayataja baadhi yake kuwa ni pamoja na Uchumi, Utamaduni, Rushwa an Maadili, Katiba na Sheria pamoja na Muungano.
Aliyataja baadhi ya maeneo muhimu ya kisiasa yaliomo kwenye ripoti hiyo na mapendekezo yaliotolewa, kuwa ni pamoja na Siasa na Demokrasia pamoja na namna ya kyaenzi Mapinduzi na Muungano.
Maeneo mengine ni Tume ya Maridhiano, Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Uteuzi wa Viongozi wa ngazi ya chini ya Serikali (masheha), Uchaguzi Mkuu, Daftari la Wapiga Kura pamoja na Kura ya Mapema.Aidha, maeneo mengine ni Matokeo ya Uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, Muungano, Mikopo ya Zanzibar kwa taasisi za Nje, Suala la Umiliki wa Mipaka ya kisiiwa cha Fungu Mbaraka, Tume ya Pamoja ya Fedha, Mgawanyo wa Nafasi za Ajira Tanzania, uteuzi wa Mawaaziri Tanzania pamoja na Ushuru wa Bidhaa za Zanzibar zinazokwenda Tanzania Bara.
Nae, Makamo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Balozi Amina Salum Ali alisema katika utekelezaji wa kazi hiyo wajumbe wa Kamati hiyo walionyesha dhamira ya kweli katika kuleta mustakabli mwema wa kisiasa hapa nchini wakati wa kuchambua maoni hayo.
Kamati Maluum ya kuchambua maoni mahsusi ya Wazanzibar iliohusisha wajumbe kutoka makundi yote, iliteuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. HusseinMwinyi Oktoba 14.