RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inafurahi kufanya kazi na wawekezaji katika miradi mbali mbali iliomo katika sekta ya Uchumi wa Buluu.Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Jijini Zanzibar alipozungumza na Ujumbe wa baadhi ya Wawekezaji kutoka Uingereza ulioongozwa na Msaidizi wa Waziri Mkuu katika masuala ya Biashara Lord Wanley, ambapo pia uliambatana na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania David Concar.

Amesema Zanzibar ina fursa nyingi za Uwekezaji katika sekta ya Uchumi wa Buluu, ikiwemo kilimo cha Mwani pamoja na uvuvi wa bahari kuu na kubainisha baadhi ya changamoto zinazokabili maeneo hayo, hususan ya ukosefu wa soko na kiwango kidogo cha bei katika zao la mwani.Aliushukuru ujio wa ujumbe huo na kusema hatua hiyo itatoa fursa kwa Kampuni mbali mbali zinazohitaji kufanyakazi katika maeneo mbali mbali yaliopo kuwekeza.

Nae, Kiongozi wa Ujumbe huo Lord Wanley alimtambulisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyi baadhi ya Wawekezaji alioambatana nao na aina ya miradi ya uwekezaji.Miongoni mwao wawekezaji hao ni wanaoshughulika na uwekezaji katika miradi ya kilimo cha mwani, ujenzi wa boti, miundo mbinu ya barabara pamoja na uwanja wa ndege.

Mapema, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Suleiman Masoud Makame, alisema ujio wa ujumbe huo ni hatua ya mwendelezo kutokana na mkutano wa Biashara kati ya Tanzania na Uingereza ambao ulifanyika nchini Novemba 16, 2021.Alisema ujumbe huo umekuja nchini kwa dhamira ya kuangalia fursa za Uwekezaji, hususan katika sekta ziliomo katika uchumi wa Buluu na maeneo mengineyo.

Alisema ujumbe huo umepanga kukutana na kufanya majadiliano na Wafanyabaishara kutoka sekta binafsi katika Hoteli ya Serena Inn.