RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesifu maendeleo makubwa ya kiuchumi yaliyofikiwa na Ufilipino kupitia sekta mbalimbali.Alisema Zanzibar ina mengi ya kujifunza kwa Ufilipino kutokana na uzoefu na weledi wa kuyafikia maendeleo hayo hasa kwenye sekta za mafuta na gasi, utalii, uvuvi na afya.Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na balozi wa Ufilipino nchini Tanzania, Marie Charlotte aliyefika kujitambulisha.
Rais Dk. Mwinyi alisema Utalii ni sekta mama kwa uchumi wa Zanzibar na kumshauri Balozi Charlotte kuangalia fursa za uwekezaji kwenye sekta hiyo kwa kuitangaza zaidi Zanzibar huko kwao.

Alisema, Zanzibar ina idadi ndogo ya raia wa Ufilipino, hivyo alimueleza balozi huyo matarajio yake kuona ushirikiano uliopo unaimarika zaidi kwa kuongezeka raia wengi wa Ufilipino, Zanzibar.Vile vile, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi huyo kwamba Zanzibar inawakaribisha raia wa Ufilipino kuja kuwekeza kwenye sekta ya Uchumi wa Buluu kwani ina mawanda mapana ya uwekezaji na faida kubwa kwa pande zote mbili za ushirikiano.

Naye, Balozi Charlotte alimueleza Rais Dk. Mwinyi wataongeza uhusiano wa kidiplomasia ulipo baina ya Tanzania na Ufilipino, nakusema kwamba ataitangaza Zanzibar kwa kusawishi wawekezaji kutoka nchini kwake kuwekeza Zanzibar kutokana na fursa zinazopatikana kwenye visiwa vyake.Pia balozi huyo, aliisifu Zanzibar na kusema mazingira yake yanafanana sana na Ufilipino na alishangazwa na utamaduni wa watu wa Zanzibar kwa ukarimu wao kwa wageni, unatofautiana kidogo na ule wa Wafilipino.

Uhusiano wa Diplomasia baina ya Tanzania na Ufilipino ulianza tangu Disemba 15 mwaka 1961 kwa pande mbili hizo kufungua ofisi za kidiplomasia na kushirikina kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo, jamii na uchumi.Ufilipino mji mkuu wake Manila, iko Kusini Mashariki mwa bara la Asia, ni nchi ya visiwa Magharibi mwa bahari ya Pasifiki, ina visiwa vidogo 7,641, inachangia mipaka na bahari ya China.