Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi leo amewaapisha viongozi mbali mbali aliowateua hivi karibuni wakiwemo Mawaziri, Manaibu Mawaziri pamoja na Makamishna.

Hafla hiyo ya uapisho imefanyika leo katika viwanja vya Ikulu Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wakuu wa Kitaifa, Mawaziri, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Kisiasa pamoja na watendaji wengine wa Serikali.

Miongoni mwa viongozi walioapishwa hivi leo ni Jamal Kassim Ali ambaye anakuwa Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais–Ikulu, Dk. Saada Mkuya Salum anayekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango. Harusi Said Suleiman anayekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.

Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Hamza Hassan Juma, Dk. Khalid Salum Mohamed anaekuwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazrui, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Riziki Pembe Juma.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Simai Mohamed Said. Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Suleiman Masoud Makame, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Rahma Kassim Ali, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Lela Muhamed Mussa, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis, Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Shaib Hassan Kaduara.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi amewaapisha Manaibu Waziri akiwemo Naibu Waziri Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi,  Juma Makungu Juma, Naibu Waziri Wizara ya Afya, Hassan Khamis Hafidh, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Ali Suleiman Ameir (Mrembo), Naibu Waziri, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Nadir Abdullatif Yussuf Alwardy, Naibu Waziri, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Abdulgullam Hussein, Naibu Waziri Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Anna Athanas Paul pamoja na Naibu Waziri, Wizara ya Maji, Nishati na Madini ambaye anakuwa Shaaban Ali Othman.

Pia, Rais Dk. Mwinyi amemuapisha Kamishna wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma Balozi Mohamemd Mwinyi Mzale pamoja na kumuapisha Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar Yussuf Juma Mwenda.

Baadhi ya viongozi walioapishwa hivi leo walifanya mahojiano na waandishi wa habari na kueleza jinsi walivyofarajika na uteuzi walioupata na kuahidi kwamba watamsaidia na kumuunga mkono Rais Dk. Mwinyi katika kuhakikisha anatekeleza vyema kiu yake ya kuiletea maendeleo endelevu Zanzibar pamoja na watu wake