SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea kutekeleza programu mbalimbali za zao la mwani Unguja na Pemba ili kuwaungamkono na kuinua juhudi za kinamama wengi wanaojishughulisha na kilimo cha zao hilo.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi aliyasema hayo wakati akizindua Mpango Mkakati wa miaka mitatu pamoja na mradi wa “Tumaini kit” kwa taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) iliyotimiza mwaka mmoja tokea kuasisiwa kwake Julai mwaka 2022. Hafla ilifanyika katika ukumbi wa Golden Tulip, Uwanja wandege Zanzibar.

Dk. Mwinyi alisema jukumu la kuleta maendeleo ya nchi, kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi, ulinzi wa watoto dhidi ya vitendo vya ukatili na kukabiliana na tatizo la udumavu kwa watoto sio la Serikali peke yeke, bali ni la kila mwananchi.“Binafsi naishukuru sana taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” kwa kuungamkono juhudi za Serekali katika kuwainua wanawake, kina mama na vijana wanaojishughulisha na kilimo cha mwani kwa kuwapa mafunzo na vifaa mlivyovitafuta kwa juhudi zenu, nasi upande wetu Serikali tutaendelea kutekeleza programu mbalimbali za zao la mwani Unguja na Pemba.” Dk. Mwinyi aliipongeza taasisi hiyo.

Alisema ZMBF imegusa maeneo umuhimu yanayoungwa mkono na Serikali kwa ustawi mkubwa wa jamii na kuwaahidi kushirikiana nao kwenye mapambano ya kumaliza kabisa vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia kwa watoto hapa Zanzibar na kuendelea kuipongeza taasisi hiyo kwa juhudi zao za kupaza sauti za waathirika kwa kupata uzito.Alisema Zanzibar Maisha Bora Foundation imegusa maeneo umuhimu yanayoungwamkono na Serikali kwa ustawi mkubwa wa jamii na kuwaahidi kushirikiana nao kwenye mapambano ya kumaliza vitendo vya udhalilishaji nchini.

Akizungumzia tatizo la udumavu kwa watoto wa Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi alieleza wastani wa watoto wawili kati ya 10 Zanzibar wamedumaa, hivyo aliipongeza taasisi hiyo kuangalia umuhimu wa lishe kwa watoto na kuweka mkazo kwenye eneo hilo ili kuwanusuru watoto wengi dhidi ya janga hilo kwa kuokoa kizazi cha baadae.Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza janga la udumavu kwa watoto linaepukika ikiwa jamii inawekeza kwenye lishe bora kwa mama wajawazito na watoto wachanga tokea wanapozaliwa hadi wanapofika umri wa miaka miwili pia aliwahamasidha kinamama kuendelea kuwanyonyesha watoto wachanga kwa miezi sita ya awali ili kupunguza na kuondosha kabisa tatizo la udumavu wa watoto nchini.

Hata hivyo Dk. Mwinyi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaungamkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na taasisi hiyo pamoja na wadau wengine katika kuboresha maisha ya Wazanzibari. Aliongeza Serikali ina wajibu kwa wananchi wake wa kuweka mazingira wezeshi na kuunganisha nguvu za wadau wote ili kusukuma gurudumu la Maendeleo ya nchi.Katika hatua nyengine, Rais Dk. Mwinyi aliupongeza maradi wa “Tumaini kit” unaotekelezwa na taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foudation wa kuzalisha taula na kike kwa wasichana uliowalenga wanafuzi wa skuli za msingi na Sekondari za Unguja na Pemba.

Alisema Serikali ina mahitaji makubwa ya taula hizo kwa wanafunzi hivyo, alipongeza dhamira ya taasisi hiyo katika kuisaidia Serikali na kueleza upatikanaji wa uhakika wa taula hizo utawapa sitara wasichana walioko skuli kwa kuwawesha kuhudhuria masomo yao bila ya kukatisha wanapokua kwenye ada zao za kila mwezi na kulinda utu wa mtoto wakike.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya ZMBF ambae pia ni Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mariam Mwinyi alisema mwaka mmoja tokea kuanzishwa kwa taasisi hiyo wamefanikiwa kuisimamisha taasisi hiyo, kuweka sawa mifumo ya uwendeshaji, kusimamia matumizi sahihi ya fedha za taasisi kwa kufanikisha vyema malengo ya taasisi hiyo, utekelezaji wa miradi iliyojipangia, ushirikishwaji wa wadau wake pamoja na kuandaa mpango mkakati wa miaka mitatu wa utekelezaji wa majukumu ya tasisi kwa mwaka 2023 hadi 2025 ambao unatarajia kutumia dola za Marekani milioni mbili ili kufanikisha malengo iliyojiwekea.

Aidha, Mama Mariam Mwinyi, alieleza taasisi hiyo inashajihisha afya ya jamii kujiepusha na maradhi yasiyoambukiza ukiwemo ugonjwa wa moyo, presha na kisukari kwa kushajihisha jamii kufanya sana mazoezi kwa nia ya kuimarisha afya zao.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohamed, alizitaka asasi nyengine za kiraia kuiga mfano wa ZMBF kwa kuwatumikia watu, kupaza sauti za wanyonge na wafikia kila penye uhitaji ili kuwa msaada mkubwa kwao.Kwa upande wake Mkurugenzi wa ZMBF, Mwanaidi Ali alieleza malengo ya kimkakati ya taasisi hiyo katika kuungamkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya nane kupitia sera yake ya kuinua uchumi wa Buluu, alisema ZMBF inafanyakazi kwa karibu zaidi kuwainua kiuchumi kinamama wanaojishughulisha na kilimo cha mwani kwa kuwasaidi vifaa na vitendea kazi kwenye shughuli zao za kilimo.

Alisema adhma ya taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu ni kutimiza malengo na mielekeo minne ya kimkakati yenye malengo makuu 11 ikiwemo kuwainua ustawi wa wananwake na vijana katika uchumi wa buluu hususani wakulima wa mwani na kuongeza kuwa ZMBF ilifanya tathmini ya awali kwa vikundi 14 vya kina mama na kuwapatia vitendea kazi vyenye thamani ya shilingi milioni 130 ikiwemo boti 17 za kisasa na vifaa vyake kwaajili ya kina mama hao.

Aidha, alieleza ZMBF inania ya kuwaendelezea mafunzo kwa wakulima hao, kuongeza thamani ya bidhaa zao na kuimarishia soko, kuimairsha lishe ya mama na mtoto na kuzalisha taulo za kike kwaajili ya wajichana walio mashuleni.Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) iliasisiwa Julai mwaka 2022 na kuzinduliwa rasmi Febuari mwaka jana, tayari imefanikiwa kuzalisha taulo za kike 5000 na kuzisambaza 500 kwa wanafunzi na wasichana wa skuli za Msingi na sekondari, Zanzibar.

Aidha, taasisi hiyo inafanya kazi kwa karibu na tasisi za Serikali zikiwemo Mahakama ya Zanzibar, Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Uchumi wa Buluu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee Wazee na watoto,  Wizara ya Habari na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda.