MKE wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi amesema kuwa dhamira iliyompelekea kuanzisha Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), ni kuweza kutumia ujuzi, maarifa na uzoefu alionao katika kuchangia ustawi wa kiuchumi, kijamii na kiafya miongoni mwa Wazanzibari hususan wanawake, vijana na Watoto.
Sambamba na hayo, aliongeza kuwa kulingana na nafasi yake katika jamii na familia akiwa Mke wa Rais wa Zanzibar na pia kama mama, dada na Shangazi anaamini yupo katika nafasi nzuri ya kufahamu majukumu muiingiliano, ambayo mwanamke anayo katika jamii hivyo, hana budi kumuwezesha kifikra, maamuzi na kiafya pia.
Mama Mariam Mwinyi ambaye pia, ni Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) aliyasema hayo leo katika sherehe za uzinduzi wa Taasisi hiyo zilizofanyika katika viwanja vya Mao Zedong Jijini Zanzibar.
Alisema kuwa Taasisi hiyo imetengeneza mkakati wake wa awali wa miaka miwili ambao utalenga katika maeneo makuu matatu ambayo ni kuwezesha wanawake wanaojihusisha na ukulima wa mazao ya baharini ikiwamo la mwani, kuchangia katika vita dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia na kuimarisha afya na lishe ya watoto na mama mja mzito.
Aidha, alisema kuwa Taasisi imelenga kuwasaidia wanawake kunufaika na Uchuni wa Buluu hususan wale wanaojishughulisha na zao la mwani ambapo itashirikiana na Serikali pamoja na wadau katika kuongeza uzalishaji bora, thamani na masoko ya zao hilo ili wanawake walio katika sekta hiyo waifanye kwa ufanisi na iwaletee tija zaidi kwao, familia zao na Taifa kwa ujumla.
Hivyo, leo ikiwa ni sehemu ya awali ya utekelezaji wa shughuli za Taasisi hiyo Mama Mariam Mwinyi aliwapatia vifaa vya kutendea kazi vikundi vinane vya akina mama wakulima wa mwani wa Unguja na Pemba, vifaa ambavyo ni mashine 16 za kusagia mwani.
Akieleza juu ya suala zima la vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto Mama Mariam Mwinyi alisema kuwa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation itafanya kazi bega kwa bega na Serikali, Wadau wa maendeleo, Asasi zisizo za kiraia na Jumuiya zinazoendesha mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.
Pia, alisema kuwa Taasisi hiyo itashirikiana na wadau mbali mbali katika kuimarisha utekelezxaji wa sheria iliyopo na pia kuimarisha uwepo wa nyumba salama zitakazohusisha pia, stadi mbali mbali na utoaji wa ushauri nasaha.
Sambamba na hayo, alieleza kuwa Taasisi itawezesha kufanya kazi na uongozi wa ngazi ya shehia, wahudumu wa afya ngazi ya jamii,katika kubuni suluhisho mbali mbali endelevu za kuimarisha lishe za watoto na mama zao.
Aliongeza kuwa wataalamu wa afya na wanasaikolojia wanahimiza kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi na kushiriki michezo mbali mbali kama hatua muhimu ya kulinda na kuimarisha afya na uwezo wa akili hivyo, alitoa rai ya kuitumia kila siku ya Jumaamosi ya mwisho wa mwezi kufanya mazoezi ambapo yeye atakuwa akifanya mazoezi na kuomba kuungwa mkono.
Mama Mariam Mwinyi aliwaalika wananchi kuweza kwenda kupata huduma mbali mbali bure za afya zilizolewa katika viwanja hivyo zikiwemo huduma za mama na mtoto, huduma za macho na kinywa, huduma za lishe bora, uchangiaji wa damu salama, pamoja na chanjo ya hiyari dhidi ya ugonjwa wa UVIKO -19.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, akitoa salamu zake za pongezi kwa njia ya simu kiwanjani hapo alimpongeza Mama Mariam Mwinyi pamoja na wale wote waliomuunga mkono katika uzinduzi wa Taasisi hiyo na kueleza kwamba jambo alilolifanya linapaswa kuungwa mkono kwani linaisaidia Serikali.
Wakati huo huo, Mama Mariam Mwinyi alipata fursa ya kutembelea mabanda mbali mbali ya maonyesho na kupata maelezo juu ya shughuli mbali mbali zinazofanywa na Serikali, Taasisi mbali mbali za kiserikali na kiraia, sekta binafsi pamoja na wajasiriamali wanawake.
Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Masoud Ali Mohammed alisema kuwa jambo alilolifanya mama Mariam Mwinyi ni jambo muhimu sana na anastahili kuwa miongoni mwa wananwake mashujaa hasa ikizingatiwa pia, jambo alilolifanya ni ibada kwani ameamua kuisaidia jamii.
Mapema Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo Mwanaidi Ali alisema kuwa Taasisi hiyo imeasisiwa na Mama Mariam Mwinyi ambayo ipo kisheria ambayo imesajiliwa rasmi mwezi Julai mwaka 2021 chini ya sheria ya usajili wa Taasisi za Kiraia Namba 06 ya mwaka 1995.
Aidha, alisema kuwa mwezi Septemba mwaka jana 2021 ilianza kazi na leo Februari 19,2022 imezinduliwa rasmi ambayo ina muundo wa uongozi na usimamzi chuni ya Bodi ya Wadhamini inayoongozwa Mama Mariam Mwinyi.
Alisema kuwa Taaisi hiyo pia, ina muundo wa kiutendaji unaoongozwa na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ikiwa ni pamoja na uendeshaji wa shughuli za kila siku za Taasisi kupitia Idara mbali mbali.
Nae Mwenyekiti wa Kamati za shughuli hiyo Dk. Suleiman Haji alieleza namna ya shughuli hizo zilivyoanza na kupongeza mwitiko wa wadau mbali mbali wa ndani na nje ya Zanzibar katika kuiunga mkono Taasisi hiyo.
Katika uzinduzi huo nyimbo maalum ya uzinduzi wa taasisi hiyo uliimbwa na msanii Vicky Kamata pamoja na burudani za tenzi zilizosomwa na wasanii akiwemo Kassim Yusuf maarufu Ziro Kasorobo.
Mapema asubuhi, Mama Mariam Mwinyi aliongoza matembezi ya kilomita sita yaliyoanza katika viwanja vya Kiembesamaki maarufu kwa Butros na kupita maeneo ya Kilimani, Miembeni, Michenzani na kumalizikia katika viwanja vya Mao Zedong Jijini Zanzibar.
Viongozi mbali mbali wanawake wa Kitaifa walishiriki katika uzinduzi huo wakiwemo wake wa viongozi walioko madarakani na wale waliostaafu, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wabunge, Wawakilishi, Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, Wakuu wa Mashirika, Asasi za Kirai, wananchi mbali mbali pamoja na wanachama wa chama cha mazoezi (ZABESA) ambapo pia, miongoni mwao walishiriki kikamilifu katika matembezi hayo ya kilomita sita.