RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendeleza ujenzi wa miundombinu imara kwa Sekta za Maendeleo nchini.Dk. Mwinyi ameeleza hayo uwanja wa Jamuhuri wa Skuli ya Sekondari Utaani Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, alipofungua skuli ya Sekondari ya wanawake ya Ghorofa tatu iliyojengwa upya na serikali baada ya kupata ajali ya kuunga moto na kuteketeza kila kitu Mwezi Machi mwaka 2022.

Alisema, ujenzi wa skuli hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya serikali iliyoitoa baada ya tukio la moto lililoteketeza skuli ya awali iliyokuwa na madasa 11 na kuahidi kujenga skuli bora zaidi ambayo kwasasa ina madarasa 41.Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameahidi kujenga dahalia kubwa ya kisasa itakayoendana na hadhi ya skuli hiyo.

Katika kuboresha haiba njema ya mandhari mpya ya eneo la skuli hiyo, Rais Dk. Mwinyi ameiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kusimamia ujenzi uliobakia wa ukumbi wa mikutano na uwanja wa michezo itakayoendana na hadhi ya mwonekano mzuri wa skuli hiyo.Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameridhia ombi la wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba la kuimarishiwa skuli ya Jadida iliopo Wete Pemba na kueleza kwamba Serikali itajenga skuli mpya ya msingi ya ghorofa pamoja.

Alisema katika hatua ya kuiboresha hadhi ya kisiwa cha Pemba, Serikali kupitia Shirika la nyumba la Zanzibar (ZHC) itafanya ukarabati mkubwa wa nyumba za maendeleo za kisiwa hicho au kujenga nyumba mpya 4,000 zenye hadhi ya juu kwa Unguja na Pemba.Akizungumzia bandari ya Wete, Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza wananchi wa kisiwa Pemba kwamba Serikali pia imedhamiria kujenga bandari ya kisasa ya Wete ambapo hatua za awali za ujenzi wa bandari hiyo zimekamilika.

Pia, Rais Dk. Mwinyi ameeleza hatua za Serikali ilivyofikia juu ya ujenzi wa bandari ya Mkoani na ya Shumba mjini.Naye, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali (WEMA), alisifu jitihada za Rais Dk. Mwinyi kwa uwekezaji mkubwa anaouendeleza wa wizara hiyo na kuahidi kupitia ushirikiano mkubwa wa Wizara hiyo utaendeleza juhudi za Mhe. Rais kwa kuzitunza skuli zote ziendelee kubakia kwenye ubora wake.

Kwa upande wake Mwakilishi wa jimbo la Wete, ambae pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Harusi Said Suleiman alimshukuru Rais Dk. Mwinyi kwa kuendelea kuboresha maendeleo ya nchi zikiwemo barabara safi za mijini na vijini, ujenzi wa skuli za ghorifa na kuimarisha huduma za jamii za afya na maji safi na salama.

Akizungumza kwenye ghafla ya ufunguzi wa Utaani Sekondari, Katibu mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdalla alisema, ujenzi wa Skuli hiyo ulianza mwezi Mei mwaka jana na uligharimu shilingi bilioni 6.2 umejumuisha madarasa 41, ofisi nne za walimu, ofisi ya mwalimu mkuu, vyoo 32, maktaba, maabara, chumba cha kompyuta na stoo.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatibu alisema, wananchi wa mkoa huo sasa wanajali zaidi maendeleo na wameachana na siasa za zamani za chuki wanaendelea kuimarisha umoja, amani na mshikamano baina yao bila kujali tofauti zao, jambo alilolisifu ni kuimarika kwa maendeleo kwenye utawala wa Dk. Mwinyi.

Akitoa salamu za Chama Cha Mapinduzi, kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Zanzibar, Dk. Muhammed Said Muhammad (Dimwa), Mkuu wa Idara ya Oganaizesheni Ofisi kuu ya chama hicho Kisiwandui, Zanzibar ambae pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM - Taifa, Omar Kilupi alisema ufunguzi wa Skuli hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho ya 2020 – 2025 ambayo tayari imepitiliza malengo iliyojipangia kuwaletea wananchi wa Zanzibar Maendeleo makubwa.