RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema jukumu la kuilinda na kuitunza amani ya nchi ni la kila mwananchi kwa ngazi zote za jamii na wala sio la Serikali peke yake.Alisema, wananchi wana wajibu wa kuhimizana kudumisha amani na utulivu uliopo kwa maslahi mapana ya taifa.
Al Hajj Dk. Mwinyi aliyasema hayo alipozungumza na waumini wa dini ya kiislamu aliojumuika nao kwenye ibada ya sala ya Ijumaa, msikiti wa Masjid Noor Kombeni, Wilaya ya Magharibi B Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema, maendeleo ya taifa lolote duniani yanategemea zaidi amani, utulivu, umoja na mshikamao wa watu lake.Al Hajj Dk. Mwinyi alieleza, amani huanzia nyumbani kwenye ngazi ya familia inayotokana na malezi bora na maadili mazuri ya jamii.Hivyo, Al hajj Dk. Mwinyi aliendelea kuihimiza jamii kuitunza amani iliyopo nchini na kuitunza kwa manufaa ya taifa na watu wake na kuendelea kuishi maisha yenye upendo na yaliyomridhia Allah (S.W).

“Amani ndiyo nguzo kuu ya mambo mengine yote ya Maendeleo, bila ya amani huwezi kuzungumzia maendeleo, Alhamdulilah nchi yetu ina amani, wananchi wana umoja, mshikamano na utulivu watu kuweza kufanya shughuli zetu za ibada na maendeleo bila hofu yoyote ni jambo la kuendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu aendelee kutudumishia amani yetu.” Alieleza Alhaj Dk. Mwinyi.

Sheikh Khalid Ali Mfaume, Katibu Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, aliitaka jamii kuwa na sifa ya insaafu, kukiri na kuridhia mazuri yote yanayoendelea nchini ikiwemo hatua maendeleo ya uchumi na jamii yaliyofikia nchini ikiwemo miundombinu ya kisasa, mawasiliano bora na huduma nyengine za jamii.Akihutubu kwenye sala hiyo, Khatibu Sheikh Abdullah Juma Mussa, alisema suala la amani limezungumzwa hadi kwenye historia ya Uislamu ambao umewafundisha waumini wake elimu ya kuwa na mafanikio mema kwenye ardhi kwa kufanya maamuzi yenye hekima na kumtambua Mwenyezi Mungu (S.W)

Alisema, Mwenyezi Mungu (S.W) alimfadhilisha mwanaadamu kuliko viumbe vyengine kwa kumpa elimu, hekma na utambuzi wa kuchanganua mazuri na mabaya ili kunusuru hali za sintofahamu ikiwemo uvunjifu wa amani kwenye jamii, hatimae aishi kwenye dunia kwa hali ya amani