Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameutaka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kukamilisha kwa haraka ujenzi wa vituo vya kisasa vya mabasi vitakavyotumika katika Mradi wa Mabasi ya Umeme, ili wananchi waanze kunufaika kikamilifu na huduma hiyo.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 23 Julai 2026, wakati wa ufunguzi wa Kituo cha Mabasi Malindi na uzinduzi wa huduma za usafiri wa umma kwa kutumia mabasi ya umeme, hafla iliyofanyika Malindi, Mkoa wa Mjini Magharibi. Amesema mradi huo unalenga kuwapatia wananchi huduma za usafiri zilizo bora, salama na za uhakika, sambamba na kuboresha mfumo wa usafiri na kuimarisha haiba ya mji.

Rais Dkt. Mwinyi amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha vyombo vya usafiri vinavyotoka maeneo ya nje ya mji vinaishia katika vituo vya mabasi vitakavyojengwa pembezoni mwa mji, huku mabasi ya umeme yakitoa huduma ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi. Ameeleza kuwa kuanzishwa kwa mabasi ya umeme ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika sekta ya usafiri, hatua itakayosaidia kuhifadhi mazingira na kupunguza uchafuzi wa hewa.

Amesema utaratibu mpya wa huduma za usafiri utatoa unafuu kwa wananchi, hususan wazee na wanafunzi, na kuwawezesha kusafiri kwa urahisi bila usumbufu. Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amezitaka mamlaka zinazohusika na miundombinu ya barabara kudhibiti uvamizi wa hifadhi za barabara, ikiwemo ujenzi wa maduka na majengo mengine unaofanywa na baadhi ya wananchi katika maeneo hayo.

Amewaomba wananchi kuendelea kuunga mkono utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuwa walinzi wa miundombinu inayojengwa katika maeneo mbalimbali kwa manufaa yao. Akizungumzia utekelezaji wa miradi mikubwa, Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kutekeleza ahadi zake katika sekta za miundombinu, maji, bandari, viwanja vya ndege, barabara, hospitali na viwanja vya michezo.

Amesema hakuna mradi wa Serikali uliosimama na kwamba kasi ya utekelezaji itaongezwa ili kufikia malengo ya kuleta maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa Zanzibar. Rais Dkt. Mwinyi amefafanua kuwa Mji wa Michezo, unaojumuisha uwanja mkubwa utakaotumika katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), unatarajiwa kugharimu dola za Marekani milioni 150, sawa na takribani shilingi bilioni 300.

Amesema mradi huo hauhusishi uwanja wa AFCON pekee, bali pia bwawa la kuogelea lenye hadhi ya Olimpiki, viwanja vya mazoezi, kumbi za mikutano na hoteli. Ameongeza kuwa Mji huo wa Michezo utachochea utalii wa michezo, kuongeza idadi ya wageni watakaoitembelea Zanzibar na kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi.

Rais Dkt. Mwinyi pia amewapongeza wananchi wanaotoa maeneo yao kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akisema ushirikiano wao ni muhimu katika kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuimarisha huduma na miundombinu. Aidha, ameipongeza ZSSF kwa kukamilisha kwa haraka ujenzi wa uwanja wa michezo kwa ajili ya watoto katika eneo lililo karibu na Kituo cha Mabasi Malindi, hatua itakayowawezesha watoto wa maeneo hayo kushiriki michezo.

Hafla hiyo pia imeambatana na uzinduzi wa kadi maalumu za usafiri, zikiwemo kadi ya dhahabu kwa wanafunzi, nyeusi kwa wazee na buluu kwa abiria wengine.