Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amefutari pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba na kuwasihi kuendelea kuiombea dua nchi pamoja na viongozi wake ili waweze kutekeleza ahadi walizowaahidi wananchi.

Hafla hiyo ya futari iliyoandaliwa na Rais Dk. Mwinyi kwa ajili ya wananchi wa Mkoa huo wa Kaskazini Pemba ilifanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Wete, Pemba ambayo ilihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Serikali, dini, vyama vya siasa pamoja na makundi maalum ya wananchi wa Mkoa huo.

Katika maelezo yake, Alhaj Dk. Mwinyi aliwasisitiza wananchi kuutumia mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kwa kuwaombea dua viongozi pamoja na kuiombea dua nchi ili izidi kupata neema na mafanikio zaidi ya kimaendeleo.

Alhaj Dk. Mwinyi pia, alitumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi kwa kuendelea kuitunza amani iliyopo nchini.

Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi aliwapongeza wananchi wote waliopata mwaliko wake wa futari na kupokea mwaliko huo na kuweza kufika kwa na kufutari nae pamoja kwa lengo la kuwa karibu na wananchi wake ambao wamewawakilisha wenzao.

Sheikh Omar Hamad Ali akitoa neno la shukurani kwa niaba ya wananchi wa Mkoa huo, alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa mwaliko wake huo alioufanya kwa wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba na kumuombea dua ili azidi kuongoza kwa amani na usalama.

Nae Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi kwa upande wake aliungana na viongozi wanawake wa kitaifa pamoja na wananchi wa Mkoa huo wa Kaskazini Pemba katika futari hiyo maalum aliyoianda Alhaj Dk. Mwinyi hapo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Pemba