Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amejumuika na waumini wa dini ya Kiislamu katika Sala ya Ijumaa iliyosaliwa katika Msikiti wa Mubarak Mazrui, uliopo Mombasa, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Akitoa salamu zake kwa waumini baada ya sala hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amewanasihi waumini wa dini ya Kiislamu na wananchi kwa ujumla kuendelea kudumisha amani, umoja, upendo na mshikamano, ili Serikali iendelee kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ajili ya kuimarisha ustawi wa wananchi.

Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa nchi ipo salama, hali inayoiwezesha Serikali kutekeleza mipango na miradi yake ya maendeleo kwa mafanikio makubwa, huku akiwahimiza kuendelea kuunga mkono juhudi hizo.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa wananchi kuvumiliana na kusameheana, akieleza kuwa misingi hiyo ni muhimu katika kudumisha amani na utulivu nchini, pamoja na kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa miundombinu, uimarishaji wa sekta ya afya, viwanja vya ndege na michezo.

Rais Dkt. Mwinyi ameendelea na utaratibu wake wa kujumuika na waumini wa dini ya Kiislamu katika Sala za Ijumaa kwenye misikiti mbalimbali mijini na vijijini.