Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesisitiza umuhimu wa madrasa kuendelea kutoa elimu bora ya dini, sambamba na kuwajengea watoto uelewa wa mafundisho wanayopokea, maadili mema na misingi sahihi ya maisha ya Kiislamu. Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 07 Agosti 2026, alipojumuika na waumini wa Dini ya Kiislamu katika Sala ya Ijumaa iliyosaliwa katika Msikiti Al Aqswaa uliopo Kiboje, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema elimu ya madrasa ina nafasi kubwa katika kumjenga mtoto kielimu, kiimani na kimaadili, hivyo ni muhimu watoto wasifundishwe kusoma pekee, bali waelekezwe pia kuelewa maana na tafsiri ya mafundisho wanayojifunza. Rais Dkt. Mwinyi amesema madrasa zina jukumu muhimu katika kujenga nidhamu, mwenendo mwema na malezi bora yatakayowasaidia watoto kuwa na msingi imara wa dini na kuchangia katika kujenga jamii yenye maadili.

Aidha, ameeleza umuhimu wa kuendelea kuwaandaa na kuwaendeleza walimu wa madrasa ili wawe na uwezo wa kufundisha kwa ufanisi na kuwajengea watoto uelewa mpana wa elimu ya dini wanayopokea. Ametoa wito kwa Serikali, viongozi wa dini, wazazi na jamii kwa ujumla kuendelea kushirikiana katika kuimarisha elimu ya madrasa na kushughulikia changamoto zinazokabili taasisi hizo.

Wakati huo huo, Rais Dkt. Mwinyi amefungua rasmi Madrasa ya Fatma, iliyopo Kiboje Mkwajuni, na kueleza matumaini yake ya kuona madrasa hiyo ikitoa mchango mkubwa katika elimu na malezi ya watoto. Rais Dkt. Mwinyi amewapongeza viongozi, wazazi, waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na mfadhili kwa juhudi zao zilizofanikisha ujenzi wa madrasa hiyo, na kuwasihi kuendelea kushikamana katika kuimarisha elimu na maadili ya Kiislamu katika jamii.