RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuchangia shilingi Milioni hamsini (50,000,000), kusaidia ujenzi wa Msikiti wa Jumuiya ya Fissabilillah Tabligh Markaz, uliopo Kidoti Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Dk. Mwinyi ametoa ahadi hiyo leo wakati alipoukaguwa na kuweka jiwe la msingi Msikiti huo unaotumika kwa shughuli za Ijitmai ambao unaendelea kujengwa kwa nguvu za wananchi.

Amesema katika kuunga mkono juhudi za kuendeleza ujenzi wa Msikiti huo atachangia kiwango hicho cha fedha pamoja na kutafuta wafadhili mbali mbali, ili kusaidia maendeleo ya ujenzi wa msikiti huo mkubwa zaidi hapa Zanzibar, ili uweze kutumika ipasavyo wakati wa Ijitmai utakapofika.

Alimshukuru Waziri Haruon kwa kauli ya kuwachangisha Mawaziri wenzake kusaidia ujenzi wa msikiti huo, ambapo kila Waziri atachangia shilingi Milioni moja na Laki tano. (1,500,000).

Dk.Mwinyi aliipongeza Jumuiya ya Fissabilillah Tabligh Markaz kwa heshima kubwa waliyompa ya kuweka jiwe la misngi la Msikiti huo..

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mohamaed Mahamoud alisema ujio wa Rais Dk. Mwinyi wa kuweka jiwe la msingi Msikiti huo utakokuwa na uwezo wa kuswaliwa na waumini wapatao 5,500, unaonyesha imani na nia njema ya Kiongozi huyo kwa wananchi wake.

Nae, Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume, alisisitiza umuhimu wa waislamu kutoa sehemu ya sadaka zao ikiwemo fedha, vifaa au nguvu zao katika kuendeleza mbele uislamu.

Katika hatua nyengine, Rais Dk. Mwinyi alisema Serikali inaazimia kujipanga vizuri ili kuhakikisha inajenga madarasa ya kutosha yatakayokidhi mahitaji ya wanafunzi waliopo maskulini.

Akizindua mradi wa madarasa manane na chumba cha waalimu katika Skuli ya Msingi Chaani , Dk. Mwinyi alisema Serikali itahakikisha kunakuwepo madarasa ya kutosha pamoja na walimu wenye sifa ili kufanikisha dhamira ya kutoa elimu bora.

Alisema Serikali itajipanga kuhakikisha inakuwa na walimu wa kutosha katika masomo ya Sayansi (Hesabu, Chemistry na Physics) ili kuinua kwango cha ufaulu wa masomo hayo..

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Simai Mohamed Said, alitumia fursa hiyo kusisitiza umuhimu wa kuwepo mashirikiano katika ya Wizara hiyo, Uongozi wa Wilaya pamoja na Halmashauri katika kuweka mazingira bora ya kiusalama katika maeneo ya skuli, sambamba na kuwataka Madereva kufuata alama za barabarani kama zinavyoelekeza.

Katibu mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Khamis alisema skuli ya msingi Chaani ilianzishwa katika miaka ya 1964, na ina jumla ya walimu 33 na madarasa 22.

Alisema Ujenzi wa madarasa hayo umegharimu jumla ya shilingi Milioni 120 ikiwa ni nguvu za wananchi, taasisi na wahisani mbali mbali na umefanyika ili kuondoa changamoto ya kuwepo idadi kubwa ya wanafunzi na hivyo kulazimika kuwepo mikondo miwili ya masomo (asubuhi na jioni).

Mbunge wa Jimbo la Chaani kupitia tiketi ya CCM Juma Usonge Hamad aliomba Serikali kusadia upatikanaji wa Walimu wa masomo ya Hesabu, Physics pamoja na Chemistry, akibainisha kuwepo matokeo mabaya ay wanafunzi katika mitihani ya Taifa.

Mapema,  akiendelea na ziara yake katika Mkoa huo wa Kaskazini Unguja na kuzungumza an wafanyabaishara wadogo wadogo, Rais wa Zanzibar na Mawenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi alisema Serikali ina azma ya kuwajengea mazingira mazuri wafanaybiashara wadogo wadogo kwa kuwajengea masoko, kuwapa vitambulisho, kupunguza kiwango cha ushuru pamoja na kuwapa mitaji , mambo aliyobainisha utaratibu wake unaendelea kufanyika.

Nao, baadhi ya wafanyabiashara wadogo wadogo, ikiwemo mama lishe, waendesha bodaboda,  na wengineo waliiomba Serikali kuwajengea mazingira mazuri ya biashara zao, kupunguza ushuru, sambamba na kuwapatia mitaji