Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt, Hussein Ali Mwinyi ameihakikishia Jumuiya ya Mawakili ya Afrika Mashariki Ushirikiano wa kina katika kuimarisha Utawala wa Sheria na Maingiliano ya Ukanda wa Nnchi za Afrika Mashariki .

Rais Dkt, Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 15 Mei 2026 alipokutana na Jopo la Mawakili wa Jumuiya hiyo wakiongozwa na Rais wa Jumuiya hiyo Nd, Ramadhan Aboubakar waliofika Ikulu Zanzibar kujitambulisha.

Rais Dkt, Mwinyi amefahamisha kuwa Tanzania ikiwemo Zanzibar inaendelea kuunga Mkono juhudi na dhamira ya Nchi za Afrika Mashariki kuwa na Umoja na Ushirikiano wa kikanda Wenye nguvu za pamoja Kiuchumi ,Kijamii na Kidiplomasia.

Amepongeza hatua ya Jumuiya hiyo ya kufanya Mkutano wao wa Mwaka Hapa Zanzibar unaotarajiwa kufanyika Mwezi Novemba 2026 kuwa ni jambo zuri ambalo mbali na kuwaleta pamoja Mawakili wa Afika pia ni wakati muhimu wa Kubaini fursa za Kiuchumi na Uwekezaji ziliopo Zanzibar kwa Washiriki wa Mkutano huo.

Rais Dkt, Mwinyi ameuelezea Ujumbe huo kuwa Zanzibar inaendelea kuwa na Mageuzi na Mabadiliko makubwa katika sekta ya Utalii kwa kuwa na Utalii wa Kumbi za Mikutano ya Kimataifa badala ya Utalii wa Fukwe uliozoeleka kwa miaka mingi.

Aidha ameihakikishia Jumuiya hiyo ya Mawakili ya Afrika Mashariki Ushikiano mkubwa katika kufanikisha Mkutano Mkuu wa Jumuiya hiyo utakaofanyika Zanzibar Mwezi Novemba 2026..

Naye Rais wa Jumuiya ya Mawakili ya Afrika Mashariki Wakili Ramadhani Aboubakar amempongeza Rais Dkt, Mwinyi kwa Mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali za Kiuchumi yanayoendelea kufanyika Zanzibar Chini ya Uongozi wake ikiwemo Miundombinu ya Barabara, Viwanja vya Ndege, Viwanja vya Michezo pamoja na kuwepo kwa hali ya Amani na Utulivu .