Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara za kisasa kwa lengo la kuibadilisha Zanzibar kuwa nchi ya kisasa.
Dkt. Mwinyi amesema hayo leo tarehe 09 Mei 2026 alipokutana na viongozi na wanachama wa CCM Mkoa wa Mjini Kichama katika mkutano maalum wa kutoa shukrani baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 uliofanyika Ukumbi wa CCM Mkoa wa Amani, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuvunjwa kwa makundi ndani ya CCM baada ya uchaguzi ili kuimarisha umoja na mshikamano ndani ya Chama, huku akiwataka wabunge, wawakilishi na madiwani kuwaunganisha wanachama. Akizungumzia uchumi wa Chama, Dkt. Mwinyi amesema CCM inapaswa kuwa na uchumi imara na kujitegemea kupitia miradi ya kisasa na yenye tija ili kuongeza ufanisi wa utendaji katika ngazi zote za Chama.
Pia amesema Serikali itaendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi, wastaafu na wazee sambamba na kuimarisha huduma na maendeleo kwa wananchi. Dkt. Mwinyi yupo katika ziara maalum ya kutoa shukrani kwa wanachama wa CCM katika mikoa ya Unguja na Pemba baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.
.jpeg)