Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, leo tarehe 12 Agosti, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Kamisaa Mkuu wa Sensa ya Watu na Makazi Tanzania Mhe. Anne Semamba Makinda, Ikulu Zanzibar
Mhe. Makinda ambaye ni Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amemtaarifu Rais Dk.Mwinyi kuwa maandalizi ya Sensa itakayofanyika mwakani mwezi Agosti mwaka 2022 yanaendelea vizuri.“Kwa Upande wa Zanzibar maeneo ya Sensa yametengwa kwa asilimia 40% mpaka sasa, na zoezi linaendelea vizuri,tunatarajia kumaliza ndani ya muda” Amesema Mh Makinda.
Aidha, Mhe. Makinda aliyeongozana na Kamisaa wa Sensa Zanzibar Balozi Mohamed Hamza, amesema Sensa ya mwaka 2022 itatumia mfumo wa uingizwaji wa taarifa kwa njia za Kidigitali huku kwa mara ya kwanza itajumuisha pia idadi ya majengo nchi nzima. Kwa upande wake Mhe. Rais Dk. Mwinyi amemhakikishia Mh.
Makinda kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa tayari kutoa ushirikiano wote utakaohitajika katika kuratibu zoezi zima la Sensa ya mwaka 2022.
Rais. Dk. Mwinyi amesema, Sensa ni zoezi muhimu kwa Serikali na wadau mbalimbali, kwani Takwimu zinazokusanywa zinatumika katika mipango mbalimbali ya maendeleo.
Katika tukio jingine, Mhe Rais. Dk. Hussein Ali Mwinyi amekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria uliiongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Prof.Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi aliyefika Ikulu Zanzibar leo Agosti 12 mwaka 2021.
Waziri Prof. Kabudi amemueleza Mhe. Rais moja ya madhumuni ya ziara yake ni azma ya Wizara ya Sheria na Katiba katika kujifunza kutoka Zanzibar juu ya namna ya uandikaji wa Sheria na matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye huduma za Kisheria