Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wanaCCM pamoja na wananchi kiswani Pemba kumchagua Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi kuwa Rais wa Zanzibar kwani ndie pekee anaeweza kuyalinda Mapinduzi ya Januari 12, 1964 pamoja na kuutunza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.Dk. Shein aliyasema hayo leo katika mkutano wa uzinduzi wa Kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kisiwani Pemba, uliofanyika katika viwanja vya Gomnani ya Kale, Chake Chake Pemba katika Mkoa wa Kusini Pemba ambao ulihudhuriwa na mamia ya wanaCCM.

Katika maelezo yake, Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alisema kuwa Dk. Hussein Mwinyi ndie pekee anaeweza kuyalinda na kuyatunza Mapindzi ya Januari 12.1964 pamoja na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na hakuna kiongozi mwengine anaeweza kutekeleza hayo miongoni mwa wale wanaogombea nafasi hiyo.Makamao Mwenyekiti huyo wa CCM alieleza kuwa Zanzibar imepata uhuru wake kupitia Mapinduzi Matukufu yaliyofanyika mwaka 1964 ambapo kipindi chote hicho hadi hivi leo CCM ndio inayoongoza dola hivyo, chama hicho kinatambua mahitaji na maisha ya wananchi hasa wanyonge.

Rais Dk. Shein alisema kuwa Dk. Hussein Mwinyi anaiweza kazi ya kuyalida Mapinduzi na kuuimarisha Muungano kwani ameshaifanya kwa kipindi kirefu kupitia nafasi za uongozi alizoitumikia ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa kipindi kirefu sambamba na kuwa Waziri katika Ofisi ya Makamo wa Rais anayeshughulikia masuala ya Muungano.Aidha, Makamo huyo Mwenyekiti wa CCM alisema kuwa siku zote chama hicho hakibahatishi kuwachagua viongozi wake katika nafasi za Urais na ndio maana katika chaguzi zote wamekuwa wakipata ushindi mkubwa, hivyo kuchaguliwa kwa Dk. Hussein Mwinyi kunaonesha wazi usshindi w akishindo kwa CCM unakuja.

Rais Dk. Shein alisema kuwa CCM imemchagua Dk. Hussein Mwinyi kuwa mgombea nafasi ya Urais kutokana na sifa zote za kuwa Rais hasa ikizingatiwa kuwa yeye anapenda haki na anaichukua rushwa kwani ni mtu safi.Pia, Rais Dk. Shein alisema kuwa Dk. Hussein Mwinyi ni mtu mwenye maadili na kiongozi mchapa kazi mahiri na mwenye elimu kubwa na mwenye utaalamu wa afya na aliyebobea katika fani hiyo kwani ni mtu anayejituma sana.Rais Dk. Shein alisema kuwa yeye mwenyewe binafsi anamfahamu sana Dk. Hussein Mwinyi kutokana na kuwa ameshawahi kufanya nae kazi wakati Rais Dk. Shein akiwa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dk. Hussein Miwnyi akiwa Waziri katika Ofisi hiyo anayeshughulikia Muungano.

Aliongeza kuwa Dk. Hussein Mwinyi ni kiongozi mwenye maadili, heshima na nidhamu ya hali ya juu na hawezi kufananishwa na wagombea wengine wa nafasi hiyo ya Urais wa Zanzibar.“Dk. Hussein ataongoza ushindi wa CCM kwani aliyepewa kapewa na wala hapokonyeki kwnai uwezo wake mkubwa sana”alisisitiza Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar.Hivyo, Rais Dk. Shein aliwataka wananchi wa kisiwa cha Pemba kutokubali kubabaishwa wala kulazimishwa kumchagua mtu asie kuwa na sifa za kuiongoza Zanzibar na badala yake wamchague kiongozi kutoka CCM.

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza matumaini yake makubwa aliyonayo kwa Dk. Hussein Mwinyi katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi mpya ya mwaka 2020-2025 kama alivyosimamia yeye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010-2015 na ile ya 2015-2020.Makamo Mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo kumuombea kura Dk. Hussein Mwinyi pamoja na wagombea wengine wote wa CCM wa kisiwani Pemba huku akitumia fursa hiyo kuwanadi wagombea Ubunge, Uwakilishi na Udiwani wa CCM wa Mikoa Miwili ya Pemba pamoja na kuwakabidhi Ilani ya chama hicho ili waende wakainadi kwa wananchi.

Nae Mgombea Nafasi ya Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi alimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuimarisha uchumi wa Zanzibar na kupelekea kukua kwa asilimia 6.8 kwa kila mwaka.Aidha, alieleza mafanikio yaliopatikana katika utekeleza wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015-2020 chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein na kuaahidi atayaendeleza katika Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 aliyokabidhiwa.Dk. Hussein alieleza haja kwa wanaCCM na wananchi kukichagua chama hicho ili kuendeleza mafanikio hayo yaliyopatikana huku akieleza azma yake ya kuyaendeleza Mapinduzi pamoja na kuutunza na kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Aidha, alitumia fursa hiyo kueleza vipaumbele vyake iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuiimarisha sekta ya uchumi wa bahari (blue economy), hasa uvuvi wa bahari kuu kwa lengo la kuinua ajira kwa vijana sambamba na kuimarisha pato la Taifa.Dk. Mwinyi alipongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Saba hatua zilizofikiwa katika kukuza uchumi sambamba na kuongeza pato la taifa kutoka thamani ya shilingi trilioni 2.4 mwaka 2015 hadi kufikia thamani ya shilingi trilioni 3.1 mwaka 2019.
Alipongeza hatua za kuongeza makusanyo ya ndani, kutoka shilingi bilioni 428.511 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 748.9 mwaka 2019 pamoja na kupunguza utegemezi wa bajeti na kufikia asilimia 5.7 na kuvuuka lengo linaloanishwa na kufikia asilimia 7.

Aidha mgombea huyo wa urais wa Zanzibar aliwaahidi wananchi hao, kama akipata ridhaa ya kuwa rais wa Zanzibar atajenga barabara kwa kiwango cha lami, zenye urefu wa kilomita 198 kwa Unguja na Pemba.“Tunaposema tunaimarisha uchumi, lazima tuangalie pia na ujenzi wa barabara, ndio ambao utarahisuisha kila kitu,’’alieleza.Pia, Dk. Hussein Mwinyi aliyaeleza mambo mengine atakayoyapa kipaumbele ikiwa ni pamoja na kuiimarisha sekta ya utalii, sekta ya uvuvi, viwanda ufugaji wa samaki, kuwasaidia wavuvi, elimu, umeme, miundombinu, kuimarisha sekta ya kilimo na sekta nyenginezo.

Dk. Hussein, alieleza kuwa atahakikisha katika kuendeleza mradi wa upatikanaji wa mafuta na gesi mikataba itakayofungwa inawanufaisha wananchi wa Zanzibar sambamba na kuhakikisha wanapata fursa kubwa ya ajira katika sekta hiyo.Alieleza kuwa katika kuhakikisha uchumi unaimarika ni lazima miundombinu ya barabara, bandari na viwanja vya ndege vyote vinaimarishwa pamoja na kuhakikisha vinapatikana vyanzo vipya vya umeme kazi ambayo ataiendeleza kwa lengo la kukuza uchumi na maendeleo ya Zanzibar.

Sambamba na hayo alieleza azma yake ya kuimarisha huduma za jamii zikiwemo elimu bora bila ya malipo hadi Sekondari, kuongeza ufaulu kwa wanafunzi na kupitia upya mitaala ya elimu ikiwemo elimu ya ufundi ili vijana waweze kujiajiri wenyewe, kuongeza udahili, fedha kwa wanafunzi vyuoni huduma za afya kuanzia msingi hadi Rufaa, kukuza bajeti ya afya, maji safi na salama.Aidha, alieleza azma yake ya kuimarisha sekta ya kilimo, viwanda, sambamba na uimarishaji wa miundombinu ya barabara Unguja na Pemba , viwanja vya ndege na bandari.

Pia, alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa kusimamia amani na utulivu huku akiahidi na yeye kwa upande wake iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar ataiendeleza kwani anatambua umuhimu wake kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa jumla.Dk. Hussein aligusia suala zima la utawala bora katika kukuza uchumi na kusisitiza suala zima la uwajibikaji na kueleza kuwa hatowavumilia wale wote waliokuwa hawawajibiki na kuhakikisha kwamba watu hawatofanya kazi kwa mazoea.

Sambamba na hayo, Dk. Hussein alieleza dhamira yake katika kuyasaidia makundi maalum ikiwa ni pamoja na kuwalinda na kuwatunza wazee, walemavu, wanawake, wasanii na wanamichezo huku akieleza mikakati itakayowekwa katika kupamabana na dawa za kulevya na unyanyasaji wa kijinsia.

Alisema, suala la udhalilishaji linaendelea kumuumiza kichwa, hivyo akiingia madarakani, tatizo hilo atalipa kipaumbele, ili kuona kundi la wanawake na watoto linaishi kwenye mazingira bora na imara.
“Kila ninapopita wananchi wa Zanzibar wanalilia suala la udhalilishaji kuwa limekuwa kubwa mno, sasa hili lazima nilifanya miongoni mwa vipaumbe vyangu,’’alieleza.
Aidha, alieleza kuwa wizi ubadhilifu wa mali ya umma, uzembe kazini vyote hivyo atavisimamia ipasavyo na kuahidi kuweka utaratibu maalum pamoja na wale atakaowachagua katika kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi.

Mapema Naibu Katibu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi alieleza kuwa mara zote Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa kikibishana kwa Sera na sio vituko huku akieleza kuwa Dk. Hussein Mwinyi ana uwezo mkubwa wa kuiongoza Zanzibar.Aidha, alitumia fursa hiyo kuieleze kwa ufupi Ilani ya Uchaguzi mpya ya mwaka 2020-2025 na kusisitiza kuwa CCM haina ubaguzi na chama hicho kitaendelea kuwahudumikia wananchi wote.

Mkutano huo ulikwenda sambamba na burudani kutoka kwa wasanii mbali mbali wa ndani ya nje ya Zanzibar wakiongozwa na msanii mwanadada machachari katika anga za Bongo Flava Nandi, Profesa Gogo na kikundi chake pamoja na wasanii wengine mbali mbali wakiwemo wale wa kizazi kipya.Katika Mkutano huo Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM aliwaomba viongozi na wanaCCM wote kusimama kwa dakika moja kwa ajili ya kumkumbuka Marehemu Salim Hassan Turky aliyekuwa mgombea nafasi ya Ubunge Jimbo la Mpendae ambae alifariki dunia usiku wa kumkia jana na kuzikwa jioni yake Kijitoupele, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Viongozi mbali mbali wa CCM walihudhuria akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pamoja na viongozi wengine wastaafu akiwemo Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Waziri Kiongozi Mstaafu Shamsi Vuai Nahodha pamoja na viongozi wengine wa CCM kutoka Zanzibar na Tanzania Bara.