Mgombea wa Kiti cha Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi, ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kujenga soko kubwa la kisasa katika eneo la Kinyasini.Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 22 Septemba 2025 alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara na wajasiriamali wa Kinyasini, Mkoa wa Kaskazini Unguja, akiwa katika muendelezo wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi.
Amesema lengo la kujenga soko hilo jipya ni kuwaandalia mazingira bora ya kufanyia biashara pamoja na kujenga eneo la kuegesha magari.Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wafanyabiashara hao kuwa Serikali ijayo atakayoiongoza itajikita katika kuwawezesha kwa kuwapatia mitaji, mikopo isiyokuwa na riba na kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya bidhaa zao.
Aidha, amesema Serikali itaongeza maradufu fedha kwa ajili ya kuwapatia mikopo nafuu wafanyabiashara na wajasiriamali, kutoka Shilingi bilioni 96 zilizotolewa katika awamu inayoisha.Rais Dkt. Mwinyi amewaomba wananchi na wafanyabiashara kumchagua yeye pamoja na wabunge, wawakilishi na madiwani, na pia kumuombea kura mgombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili chama hicho kiendelee kuleta maendeleo zaidi.
Rais Dkt. Mwinyi amewasisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura ifikapo tarehe 29 Oktoba 2025.Wakati huohuo, akizungumza na vijana na wajasiriamali wa sekta ya utalii wa Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali inalenga kuimarisha sekta ya utalii ili kuwanufaisha wananchi wengi zaidi kupitia sera ya Utalii kwa Wote.
Amesema Serikali itajenga miundombinu ili shughuli za utalii zifanyike katika mazingira bora zaidi. Pia itatoa mitaji kupitia mikopo isiyo na riba pamoja na mafunzo kwa wajasiriamali wa sekta ya utalii watakaopata mikopo, ili kuhakikisha fedha watakazokopeshwa zinatumika ipasavyo.
Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa Serikali ijayo itajenga Serikali za Mitaa madhubuti ili kusimamia majukumu yao ipasavyo.