Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameihakikishia Jumuiya Zawiyatul Qadiriya Tanzania kuendelea kupata ushirikiano wa Serikali katika kutekeleza majukumu yake ya kuimarisha malezi, maadili na elimu ya Dini ya Kiislamu katika jamii.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 04 Agosti 2026, alipokutana na ujumbe wa viongozi wa Jumuiya hiyo, ukiongozwa na Mlezi mpya, Sheikh Ali Juma Mpwani, wakiambatana na Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Hassan Othman Ngwali, waliofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo maalum.
Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza Jumuiya hiyo kwa kazi inayofanya katika malezi ya Kiislamu kwa watoto na vijana, kusimamia na kuendesha misikiti na madrasa, kutoa elimu ya dini pamoja na kuwaandaa walimu wanaofundisha katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, ameshauri kuendelezwa kwa vikao na mawasiliano ya karibu baina ya Serikali na Jumuiya hiyo ili kuimarisha ushirikiano, kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kushughulikia mahitaji mbalimbali yanayoikabili Jumuiya, yakiwemo ujenzi wa misikiti, madrasa, vituo vya elimu ya dini pamoja na huduma za kijamii na afya.
Kwa upande wake, Mlezi mpya wa Jumuiya Zawiyatul Qadiriya Tanzania, Sheikh Ali Juma Mpwani, amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa ushirikiano na mchango anaoutoa katika maendeleo ya Jumuiya hiyo.
Sheikh Mpwani amemhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kuwa Jumuiya hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kutekeleza majukumu yake, kuimarisha malezi ya Kiislamu na kuchangia katika kudumisha maadili, amani na mshikamano katika jamii.
