Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuboresha miundombinu ya uzalishaji, matumizi ya teknolojia za kisasa, mifumo ya umwagiliaji, upatikanaji wa mikopo nafuu na masoko ya mazao ya kilimo.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 23 Septemba 2026, wakati akifungua Tamasha la Tatu la Kilimo Hai Zanzibar (Zanzibar Organic Festival 2026), Dole Kizimbani, Wilaya ya Magharibi “A”, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema Serikali inalenga kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji wa chakula kwa gharama nafuu, huku wakihifadhi rutuba ya udongo, vyanzo vya maji na mazingira, pamoja na kuhakikisha usalama wa chakula na afya za walaji.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali imezindua Mkakati wa Kilimo Hai wa Zanzibar, na ameiagiza Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kuanza mchakato wa kuanzisha Kitengo Maalum cha Kilimo Hai kitakachoratibu shughuli za kilimo hai Zanzibar.
Aidha, ameielekeza Wizara hiyo kutathmini uwezekano wa kujumuisha pembejeo za kilimo hai katika mpango wa ruzuku ya pembejeo, huku akisisitiza matumizi salama na sahihi ya pembejeo za kilimo.
Akizungumzia uhusiano wa kilimo na utalii, Rais Dkt. Mwinyi amezihimiza hoteli, mikahawa na wasambazaji wa chakula kuongeza ununuzi wa mazao yanayozalishwa na wakulima wa Zanzibar kupitia mfumo wa Shambani hadi Mezani , hatua itakayosaidia kuwaongezea wakulima masoko na kipato.
Tamasha hilo limebeba kaulimbiu “Fikiri Kiulimwengu, Kula Kiasili”, likilenga kuwakutanisha wakulima na wadau mbalimbali, kubadilishana maarifa na teknolojia, pamoja na kuhamasisha matumizi ya mbinu bora na endelevu za uzalishaji wa chakula.
Katika tamasha hilo, Rais Dkt. Mwinyi ametoa tuzo kwa wadau na wadhamini mbalimbali wanaounga mkono juhudi za kuendeleza sekta ya kilimo, na ametunukiwa tuzo ya heshima kwa kutambua uongozi na mchango wake katika maendeleo ya kilimo Zanzibar.
