Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali imeamua kuweka mfumo wa camera za usalama barabarani ili kudhibiti ongezeko la ajali zinazotokana na uvunjifu wa sheria za barabarani na kutozingatiwa kikamilifu kwa matumizi sahihi ya barabara na alama za usalama.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia Viongozi Wakuu wa Kitaifa iliyofika Ikulu leo, tarehe 10 Agosti 2026, na kuonana naye kwa mazungumzo maalum, ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Machano Othman Said.
Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa dhamira kuu ni kurudisha nidhamu barabarani, kufuatwa kwa sheria na kumfanya kila mtumiaji wa barabara kuwa katika mazingira salama wakati wote, wakiwemo madereva na watembea kwa miguu, kuwa katika mazingira salama.
Rais Dkt. Mwinyi amefahamisha kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mfumo wa camera zinazowekwa barabarani katika maeneo yote mjini na vijijini, baada ya kuanza utekelezaji huo katika Mkoa wa Mjini Magharibi, na kuwasisitiza wananchi kuunga mkono dhamira ya Serikali na hatua zinazochukuliwa na Serikali hivi sasa.
Akizungumzia suala la ajira kwa vijana, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali imekuwa ikichukua juhudi kubwa za kutengeneza miundombinu ili wananchi waweze kujituma na kujipatia kipato na kukidhi maisha yao ya kila siku, na kusisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuelimishwa kuwa ni lazima wawe tayari kujituma kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
Rais Dkt. Mwinyi amesema ni lazima vijana kubadilika kifikra na kufanya kazi kwa bidii ili kufaidika na miundombinu iliyopo hivi sasa katika maeneo mbalimbali.
Akizungumzia kupanda kwa bei za bidhaa, amesema Serikali imeendelea kuweka bei elekezi kwa wafanyabiashara kwa lengo la kudhibiti upandaji wa bei, hivyo wafanyabiashara wanapaswa kuzifuata ili kuwapunguzia wananchi hali ngumu ya maisha.
Aidha, Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuviimarisha vituo vya amali ili kuwajengea uwezo vijana na kuwa na ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kuajirika.
Rais Dkt. Mwinyi amesema kupitia Wizara ya Elimu, Serikali inakusudia kufanya mageuzi makubwa katika elimu inayotolewa katika vyuo vya mafunzo ya amali ili kuwapatia vijana stadi za ujuzi na maarifa kwa lengo la kuhimili ushindani katika soko la ajira.
Kuhusiana na mahitaji ya watu wenye ulemavu, Rais Dkt. Mwinyi ametoa agizo kwa wakandarasi na wasimamizi wa majengo kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu ili nao wapate urahisi wa kuzifikia huduma na mahitaji yao katika majengo ya sekta ya umma na sekta binafsi.
Akitoa ufafanuzi juu ya uhifadhi wa nyaraka, hoja iliyowasilishwa na Kamati hiyo, amesema upo ulazima wa kufanya mageuzi makubwa katika uhifadhi wa nyaraka za umma.
Amesema Serikali inajipanga kuhakikisha uhifadhi wa nyaraka unakuwa wa kisasa kuendana na teknolojia ya wakati uliopo na kuziwezesha nyaraka hizo kudumu kwa muda mrefu.
Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza kazi inayofanywa na Kamati hiyo ya Kusimamia Viongozi Wakuu wa Kitaifa, kwamba Serikali itaendelea kushirikiana nayo kuhakikisha majukumu ya Kamati hiyo yanatekelezeka kwa ufanisi na kufikia malengo ya Serikali Kuu na Baraza la Wawakilishi.
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Machano Othmani Said, amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa maono na utekelezaji wake wa vitendo katika kusimamia maendeleo ya nchi na kuahidi kuwa Kamati hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi hizo ambazo zimekuwa chachu ya kuleta mabadiliko makubwa ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Zanzibar katika sekta mbalimbali.
.jpeg)