Mke wa Rais wa Zanzibar, Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mhe. Mama Mariam Mwinyi, amekutana na viongozi wa Jumuiya ya Wauguzi Zanzibar (ZANA) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa ZANA, Aziza Hamed, leo tarehe 29 Julai 2026 Katika Ofisi za Migombani na kufanya mazungumzo kuhusu kuimarisha sekta ya afya, hususan juhudi za kupunguza vifo vya mama na mtoto Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Mariam Mwinyi amepongeza dhamira na maono ya ZANA ya kuwawezesha wauguzi, kuimarisha elimu ya afya na kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi. Amesisitiza kuwa uwekezaji kwa wauguzi na wataalamu wa afya ni uwekezaji muhimu unaochangia ustawi wa akina mama, watoto na jamii kwa ujumla.
Aidha, Mhe. Mariam Mwinyi amewashukuru viongozi wa ZANA kwa kumtembelea na kwa kumuamini kuwa Mlezi wa Jumuiya hiyo, akiahidi kuendelea kushirikiana nao katika kuunga mkono jitihada zinazolenga kujenga Zanzibar yenye huduma bora za afya na mustakabali salama kwa kila mama na mtoto.
