Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameishukuru Serikali ya Sweden kwa misaada yake ya maendeleo kwa Zanzibar, pamoja na kueleza umuhimu wa kuimarisha zaidi uhusiano baina ya pande hizo mbili, hususan katika sekta za biashara na uwekezaji.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 14 Julai 2026, alipokutana na Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mhe. Charlotta Ozaki Macias, aliyefika Ikulu Zanzibar kwa ajili ya kuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini.

Rais Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar inahitaji wawekezaji zaidi, huku Serikali ikiwa tayari imeweka mazingira rafiki na yenye kuvutia uwekezaji katika sekta mbalimbali za kiuchumi, hususan nishati ya umeme, kilimo cha mwani na uchumi wa buluu.

Akizungumzia sekta ya nishati, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali inaendelea na juhudi mbalimbali za kuendeleza vyanzo mbadala vya nishati, ikiwemo matumizi ya nishati ya upepo na jua. Aidha, ameyakaribisha makampuni yenye uwezo kutoka Sweden kuwekeza Zanzibar ili kuimarisha uzalishaji wa umeme na kuiwezesha Zanzibar kujitegemea katika sekta hiyo.

Rais Dkt. Mwinyi amesema sekta ya Uchumi wa Buluu ni miongoni mwa sekta kuu zinazochochea ukuaji wa uchumi na kuwashirikisha wananchi wengi. Hivyo, Serikali imeweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha zao la mwani linawanufaisha zaidi wakulima kwa kuliongezea thamani na kulitafutia masoko ya uhakika. Amesema kwa muda mrefu Zanzibar imekuwa ikisafirisha mwani kama malighafi, hali ambayo haijawaletea tija ya kutosha wakulima. Kwa msingi huo, Serikali imejipanga kuongeza thamani ya zao hilo kwa kulisarifu na kuzalisha bidhaa mbalimbali zitokanazo na mwani.

Rais Dkt. Mwinyi ameendelea kuishukuru Serikali ya Sweden kwa ushirikiano na misaada yake ya maendeleo kwa muda mrefu, hususan katika sekta za elimu, afya na ustawi wa jamii. Aidha, ameiomba Sweden kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kutekeleza malengo ya Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050.

Naye Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mhe. Charlotta Ozaki Macias, amempongeza Rais Dkt. Mwinyi na wananchi wa Zanzibar kwa hatua muhimu iliyofikiwa ya uwasilishaji wa Tamko la Pamoja na utiaji saini wa Ajenda za Kuchukuliwa Hatua baina ya Chama Cha Mapinduzi na ACT-Wazalendo.