Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za kifedha pamoja na sekta binafsi ili kuongeza upatikanaji wa mikopo ya nyumba na kuwezesha wananchi kupata makaazi bora na yenye gharama nafuu.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 25 Novemba 2026, alipokutana na ujumbe wa Shirika la Ufadhili wa Mikopo ya Nyumba Tanzania (TMRC), Ikulu Zanzibar.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na TMRC na taasisi nyingine za fedha katika kuweka mifumo madhubuti ya ufadhili itakayochochea uwekezaji, ujenzi na ukarabati wa nyumba pamoja na kupanua fursa za wananchi kupata mikopo ya muda mrefu.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TMRC, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Ndugu Theobald Sabi, amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali, benki na wadau wa sekta ya fedha kupanua upatikanaji wa mikopo ya nyumba Zanzibar ili wananchi wengi zaidi wanufaike na huduma hizo.
Ameeleza kuwa benki mbalimbali tayari zinashirikiana na TMRC katika kutoa mikopo ya nyumba, huku shirika hilo likiendelea kutafuta suluhisho la changamoto za sekta hiyo na kuimarisha upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu.
