Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na Mabalozi wa Ufaransa, Misri na Afrika Kusini wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania, leo tarehe 23 Novemba 2026, Ikulu Zanzibar. Mabalozi hao ni Balozi wa Ufaransa, Mhe. Dkt. Jean-Baptiste Jeangène Vilmer; Balozi wa Misri, Mhe. Rania Abdel-Meguid; na Balozi wa Afrika Kusini, Mhe. Noluthando Mayende-Malepe.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuimarisha ushirikiano wa Zanzibar na nchi hizo katika sekta za utalii, uwekezaji, elimu, afya, miundombinu, nishati, kilimo na Uchumi wa Buluu. Akiwa na Balozi Jeangène Vilmer, ameeleza umuhimu wa kuwajengea vijana ujuzi wa vitendo katika sekta ya utalii na hoteli, pamoja na kuvutia uwekezaji katika nishati mbadala na sekta nyingine za uzalishaji.
Kwa upande wa Balozi Rania Abdel-Meguid, Rais Dkt. Mwinyi ameomba kuimarishwa kwa ushirikiano wa huduma za kibingwa za moyo kupitia ziara za madaktari bingwa Zanzibar, pamoja na kupanua ushirikiano katika utalii na uwekezaji. Aidha, amemshukuru Balozi Noluthando Mayende-Malepe kwa mchango wake katika kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini, akisisitiza umuhimu wa kuhifadhi historia ya pamoja ya mapambano ya ukombozi.
Mabalozi hao wameonesha utayari wa kuendeleza ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika maeneo mbalimbali ya maendeleo.
