Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali inatarajia kuanzisha shirika la ndege ili kuongeza ushindani katika sekta ya usafiri wa anga, kupunguza gharama za nauli na kurahisisha safari kati ya Zanzibar na Arusha, hatua itakayowanufaisha wananchi na Watalii na kuimarisha Muunganiko wa maeneo hayo mawili.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 17 Novemba 2026, alipokutana na Madiwani wa jiji la Arusha wakiongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Paul Makonda, Ikulu Zanzibar, ambapo walijadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na Arusha katika sekta mbalimbali za maendeleo. Viongozi hao pia wamemshukuru Rais Dkt. Mwinyi kwa mapokezi mazuri waliyopatiwa wakati wa ziara yao.

Dkt. Mwinyi amesema mpango huo utasaidia kuunganisha kwa karibu zaidi maeneo hayo mawili yenye nafasi muhimu katika sekta ya utalii nchini, na kufungua fursa zaidi za biashara, uwekezaji na ajira.

Amesema ushirikiano huo unapaswa pia kutumika katika kubadilishana uzoefu na kuendeleza shughuli za maendeleo zenye manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili.

Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kuwahamasisha wawekezaji waliopo Zanzibar kuangalia fursa za Arusha na wale wa Arusha kuwekeza Zanzibar, hususan katika huduma za malazi na shughuli nyingine zinazohusiana na utalii.
Pia ameitaka Bodi ya Utalii Tanzania na Kamisheni ya Utalii Zanzibar kushirikiana katika kutangaza vivutio kwenye maonesho ya kimataifa na kuandaa vifurushi vya pamoja vitakavyowawezesha watalii kutembelea Zanzibar na Arusha katika safari moja.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuongeza uwezo wa sekta ya utalii na kukidhi ongezeko la wageni wanaotembelea visiwa hivyo.

Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar imekuwa ikipokea zaidi ya watalii laki moja kwa mwezi katika kipindi cha karibuni, sambamba na kuongezeka kwa wawekezaji wanaoonesha nia ya kuanzisha miradi mipya ya hoteli, ikiwemo katika Kisiwa cha Pemba.

Rais Dkt. Mwinyi amesema pia utalii wa ndani una mchango mkubwa katika uchumi wa Zanzibar, huku wananchi wengi kutoka Tanzania Bara wakitembelea visiwa hivyo, jambo linaloongeza mahitaji ya usafiri, malazi na huduma nyingine.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Paul Makonda, amesema ziara ya viongozi wa jiji la Arusha Zanzibar inalenga kujifunza na kubadilishana uzoefu katika sekta ya utalii na kuboresha huduma zinazotolewa kwa wageni wanaotembelea maeneo mbalimbali nchini.

Amesema hatua hiyo inaunga mkono dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuongeza idadi ya watalii na manufaa yatokanayo na sekta hiyo.