Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuimarisha ushirikiano wa biashara, uwekezaji, utalii, usafiri wa anga na Uchumi wa Buluu na Jamhuri ya Kenya ili kuongeza fursa za kiuchumi na ustawi wa wananchi wa mataifa hayo mawili. Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 27 Julai 2026, Ikulu Zanzibar, alipokutana na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Catherine Karemu, aliyefika kujitambulisha rasmi kufuatia kuanza majukumu yake nchini.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amesema uhusiano wa Tanzania na Kenya ni wa kihistoria na kidugu, na umeendelea kuwa msingi muhimu wa kuimarisha biashara, uwekezaji na ushirikiano katika sekta mbalimbali za maendeleo. Aidha, amesisitiza umuhimu wa taasisi zinazosimamia viwango katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kushirikiana kwa karibu ili kurahisisha biashara, na kuongeza ushindani wa bidhaa katika soko la kikanda.
Rais Dkt. Mwinyi amesema kukamilika kwa ujenzi wa Bandari ya Shumba, Pemba, pamoja na kuongezeka kwa safari za ndege za moja kwa moja kati ya Zanzibar na Kenya, kutaimarisha usafirishaji wa watu na bidhaa, kuongeza biashara, kukuza utalii na kuvutia uwekezaji zaidi. Vilevile, ameyakaribisha makampuni binafsi ya Kenya kutumia fursa zilizopo Zanzibar katika sekta za utalii, Uchumi wa Buluu, kilimo cha mwani na maeneo mengine ya kimkakati yanayochangia ukuaji wa uchumi na ajira.
Kwa upande wake, Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Catherine Karemu, ameahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya Kenya na Tanzania, hususan Zanzibar, kwa kuendeleza fursa za biashara, uwekezaji na maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa mataifa hayo mawili.
.jpeg)