Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema utekelezaji wa Ilani ya CCM Zanzibar unaendelea vizuri, huku miradi mbalimbali ya maendeleo ikitekelezwa na baadhi ya malengo yaliyowekwa yakivukwa.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 10 Novemba 2026, alipokutana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Ndugu Aggrey Mwanri, Ikulu Zanzibar, na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya Chama na Serikali ili kuhakikisha malengo ya Ilani yanafikiwa hadi mwaka 2030.

Aidha, amempongeza Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Asha-Rose Migiro, kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Afrika (CAPP), akiwakilisha Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, Ndugu Aggrey Mwanri amepongeza kasi ya maendeleo Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi, akieleza kuwa utekelezaji wa Ilani unaonekana kupitia miradi inayogusa maisha ya wananchi na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.