RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema suala la umiliki wa ardhi hapa Zanzibar lilitokana na tamko la Rais wa kwanza wa Zanzibar, Marehemu Abeid Amani Karume, katika ‘Manifesto’ ya uchaguzi ya Chama cha Afro Shirazi ya mwaka 1963.
Dk. Shein amesema hayo Dundua Bumbwini, Mkoa wa Kaskazini Unguja, katika ufunguzi wa nyumba za makaazi kwa wananchi waliopisha mradi mkubwa wa ujenzi wa Bandari ya mafuta na gesi asilia katika eneo la, hafla ambayo pia ilihusisha na Uwekaji Jiwe la msingi la msikiti pamoja na Lango kuu la kuingilia Bandarini.
Amesema kupitia Ilani ya ASP Marehemu Mzee Karume alitangaza ardhi yote ya Zanzibar kuwa mali ya Serikali na kueleza sheria ya Ardhi zimebainisha kuwa Serikali itaweza kuchukua eneo lolote la ardhi zinazoendelezwa na wananchi kwa shughuli za maendeleo.
Alisema Sheria ya Ardhi ya mwkaa 1992 imeweka utaratibu wa matumizi na kubainisha Zanzibar kuwa miongoni mwa nchi zenye sheria bora za ardhi Barani Afrika.
Alisema pale Serikali itakapoona ipo haja ya kutumia ardhi yake kwa shughuli za maendeleo haitosita kufanya hivyo na kuwalipa fidia wananchi kutokana na rasilimali zilizopo pamoja na vipando, jambo ambalo limefanyika huko kijiji cha Dundua.
Aidha, akinasibisha kauli yake na hatua ya wananchi wachache waliopingana na uamuzi wa serikali wa kuondoka katika maeneo yao kupisha ujenzi wa Bandari ya Mafuta na Gesi asilia, Dk. Shein alisema kamwe Serikali haiwezi kugombana na wananchi wake, hali iliomfanya kuwaagiza Mawaziri kukutana na wananchi w akijiji hicho na kuwaeleza juu ya umuhimu wa mradi huo kwa maendeleo yao na Taifa.
Alieleza kuwa Dundua ni Wazanzibari wote na hakuna mtu yeyte atakaebaguliwa ; akibainisha jitihada zilizochukuliwa na Serikali zina lengo la kuijenga nchi na kusema yale yote yaliopangwa kufanyika hayana budi kukamilishwa.
Aliwataka wananachi wote waliopata fursa ya kuishi katika nyumba hizo za kisasa kufuata taratibu za ujenzi na kusisitiza umuhimu wa kudumisha usafi ndani na nje ya nyumba zo pamoja na kuziweka katika mazingira bora.
Aidha, aliwata kujifunza namna ya kuanzisha bustani zenye kuleta tija na haiba, kwa kuotesha vipando mbali mbali ili kupata chakula, sambamba na kutoa indhari katika kukabiliana na magonjwa mbali mbali, yakiwemo yanayosababishwa na mbu.
Dk. Shein aliwataka wananchi hao kujifunza juu ya matumizi sahihi ya gesi kwa ajili ya kupikia kwa kigezo kuwa matumizi ya kuni hayaendani na uhalisia au ubora wa nyumba hizo.
Akizungumzia sababu ya kuanzishwa ujenzi wa nyumba hizo, alisema unalenga kubadilisha mwelekeo wa uchumi wa Zanzibar kwa serikali kuwekeza nguvu zake katika Uchumi wa Buluu (blue Economy).
Alisema ili kufikia dhamira hiyo kunahitajika kuwepo miundombinu miwili muhimu, ikiwemo ule wa ujenzi wa Bandari ya kisasa ya Mpigaduri pamoja na Bandari ya Mafuta na Gesi asilia katika eneo Mangapwani.
Alisema wakati wa kuanza kwa mradi wa Ujenzi wa Bandari ya mafuta na gesi asilia kulikuwa na watu wenye mitizamo tofauti ikiwemo waliopinga, hata hivyo akabinisha kuwa Serikali imetenga eneo la ardhi la kilomita saba kuendeleza mradi huo.
Aliipongeza Kamati ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kazi kubwa ya kusimamia uendelezaji wa wa mradi huo pamoja na hatua mbali mbali ilizozichukuliwa.
Alisema baada ya tafiti kubainisha kuwepo maeneo ya miamba yenye uwezo wa kuhifadhi mafuta na kuleta matumaini makubwa hapa nchini, ni muhimu kwa kijiji cha Dundua kilicho jirani na bandari hiyo kuwa cha kisasa ili wakaazi wake waweze kuishi vizuri.
Alisema baada ya ujenzi wa nyumba hizo kumalizika, ni vyema kwa wakaazi wake kuhamia hivi sasa kwa msingi kuwa zina huduma zote muhimu, hivyo sio busara wakaazi hao kutoa sababu zitakazowachelewesha kuhamia.
Aidha, Dk. Shein alisema Serikali iliagiza maeneo yote ya asili ikiwemo makaburi yaendedelea kubaki kama yalivyo (bila kuharibiwa) pamoja na wananchi kuendeleea kulitumia eneo hilo la makaburi kwa kuzingatia Serikali haiwezi kudharau tamaduni na imani za watu.
Vile vile, alisema uamuzi wa kujenga msikiti na madrasa katika eneo hilo umefanywa ili kuwawezeshaa wakaazi wake kufanya ibada pale watakapohamia katika nyumba hizo.
Katika hatua nyengine, Rais Dk. shein alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kuchagua viongozi wenye uwezo, waadlifu, wenye busara na watakaoshirikiana na serikali, katika uchaguzi mkuu baadae mwaka huu, kwa kigezo kuwa ndio watakaofanikisha ujenzi wa Bandari hiyo, sambamba na kuchochea maendeleo na kuifanya kufumbuka zaidi.
Dk. Shein aliyapongeza mashirka na taasisi mbali mbali za serikali, ikiwemo Mamlaka ya maji na nishati Zanzibar (ZURA), Mamlaka ya maji Zanzibar (ZAWA), Shirika la Umeme (ZECO) kwa kufanya kazi kubwa na kuzitaka kuendelea kushirikiana katika kazi zote za Serikali na hivyo kuleta mabadiliko na haiba katika miji mbali mbali hapa nchini.
Nae, Waziri wa Ardhi, Nyumba Maji na Nishati Salama Aboud Talib alisema kamati ya Mawaziri wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilifanya kazi kwa mashirikiano makubwa ili kuhakikisha kijiji hicho kinajengwa kwa mafanikio.
Alimpongeza Rais Dk. Shein kwa rai yake ya kuwajengea nyumba za makaazi wananchi waliopisha ujenzi huo wa bandari ya mafuta na gesi badala ya kuwakabidhi fedha zao mkononi.
Aidha, alivipongeza vikosi vya KMKM na Mafunzo pamoja na wadau mbali mbali waliojitokeza kwa kufanya kazi kwa moyo na kufanikisha dhamira na malengo ya serikali.
Mapema, Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Ali Halil Mirza alisema ujenzi wa kijiji kipya cha Dundua uliohusisha nyumba 31 umefanikishwa kwa ushirikiano wa Vikosi vya KMKM , Mafunzo na Wakala wa Majengo na kugharimu zaidi ya shilingi Bilioni 1.56 , sambamba na kuhusisha majengo mbali mbali ya huduma za kijamii, ikiwemo msikiti, madrasa na soko.
Alisema ujenzi wa kijiji kipya cha makaazi Dundua ni Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwkaa 2015-2020.
Alisema ujenzi wa Bandari ya Mafuta na Gesi asilia katika eneo hilo utachangia na kuimarisha harakati za kiuchumi pamoja na kuchochea maendeleo.
Aidha, Katibu Mkuu huyo aliwataka wananchi wa Dundua kuzipokea nyumba hizo na kuzitunza ili ziweze kudumu kwa muda mrefu.
Katika risala yao, iliyosomwa na Haji Twaha Makamae, wananchi wa Dundua walisema wameamua kukubaliana na uamuzi wa Serikali wa kupisha mradi wa ujenzi wa Bandari ya mafuta na gesi asilia katika eneo lao kwa minajil ya kuleta maendeleo.
Waliomba Serikali kuandaa kumbu kumbu zote za asili pamoja na kumbu kumbu za makubaliano kati yao, sambamba na kuomba kupatiwa eneo jengine kwa shughuli za kijamii, ikiwemo kilimo.
Aidha ,wameomba kupatiwa ajira za kudumu ili kuondokana na hali ngumu ya maisha pamoja na kupatiwa vifaa vya uvuvi.