Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kuimarisha mifumo ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, endelevu na zinazopatikana kwa usawa.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 27 Julai 2026, Ikulu Zanzibar, alipokutana na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania Mhe. Nicole Providoli.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali inaendelea kujenga taasisi imara za afya, kuimarisha mfumo wa ugharamiaji wa huduma za afya na kutekeleza Bima ya Afya kwa Wote ili kuongeza upatikanaji wa huduma bora na kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa wananchi.

Aidha, ameishukuru Serikali ya Uswisi kwa ushirikiano wake wa muda mrefu katika sekta ya afya, hususan katika utafiti, mapambano dhidi ya malaria na kuimarisha mifumo ya utoaji na ugharamiaji wa huduma za afya.

Kwa upande wake, Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Mhe. Nicole Providoli, amesema Uswisi itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya, ikiwemo utafiti, mifumo ya afya, ugharamiaji wa huduma na juhudi za kutokomeza malaria kwa manufaa ya wananchi.