Media » News and Events

Alhadj Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itahakikisha inasimamia kikamilifu masharti yote yatakayowekwa na Serikali ya Saud Arabia

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akimpa Mkono wa Eid Bw. Mohammed Ali Mzee, katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhadj Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itahakikisha inasimamia kikamilifu masharti yote yatakayowekwa na Serikali ya Saud Arabia ili kuwawezesha mahujaji wa Zanzibar kushiriki Ibada ya Hijja baadae mwaka huu (2021).Alhadj Dk. Mwinyi amesema   hayo katika hotuba aliyoitowa kwa wananchi waliohudhuria Baraza la Eid el Fitri, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakil Jijini Zanzibar.

Amesema baada ya waislamu wa Zanzibar kushindwa kutekeleza ibada ya Hijja mwaka 2020 kutokana na zuio lililotokana na Ugonjwa wa Covid 19 ulioikumba Dunia, Serikali inakusudia kusimamia kikamilifu safari ya mahujaji hao mwaka huu, kwa kuhakikisha mahujaji wanatekeleza kikamilifu masharti yatakayotolewa na Serikali ya Saudi Arabia, ili kufanikisha ibada hiyo.

Alisema Serikali itatowa taarifa za kina kuhusiana na safari hiyo, huku akiwataka waislamu waanofanya kazi kujiandaa na Ibada hiyo mapema, badala ya kusubiri hadi wanapostaafu.

Aidha, aliitaka Kamisheni ya wakfu na Mali ya Amana kukamilisha mapendekezo yaliotolewa ya kuanzisha Mfuko wa Hijja Zanzibar, ili kuwawezesha Mahujaji wa Zanzibar kutumia Mfuko huo na kufanikisha safari hizo, ili kuusukuma mbele uislamu.

Rais Alhadj Dk Mwinyi, amewataka waislamu kudumu katika maisha yanayozingatia uadilifu pamoja na kujiepusha na mambo ya batili.

Alisema kupitia Aya mbali mbali za – Qor-an Mwenyezi Mungu amewahimiza waja wake kuishi katika maisha yanayozingatia uadilifu, ikiwa ni njia sahihi ya kupata ufanisi katika mambo mbali mbali.

Alisema uadilifu ni miongoni mwa mambo ya msingi ambapo waislamu waliweza kujifunza katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kila mmoja kuheshimu haki za mwengine, hivyo akawataka waislamu kujitahidi sana kudumu na jambo hilo.

“……….tunafundishwa kuwa , hili ni miongoni mwa mambo aliyowapa Mitume ambao ndio viongozi wetu ni kusimamia uadilifu kwa watu waliokuwa wakiwaongoza”, alisema.

Alisema kila muislamu wakiwemo viongozi wa serikali, taasisi, jamii na hata familia ana wajibu wa kudumisha msingi huo, akibainisha kuwa jambo hilo litakapoendelezwa litaimarisha utoaji wa haki na usawa katika utoaji huduma, ikiwa ni msingi muhimu katika sheria na Utawala bora.

Aidha, Rais Alhadj Dk. Mwinyi alisema wakati huu waislamu wakisherehekea sikukuu ya Eid el Fitri, wana wajibu wa kuwajali na kuwasaidia waislamu wenzao waliojaaliwa kuwa na uwezo mdogo wa kipato.

Alieleza kuwa katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan, jamii hiyo iliishi kwa kushirikiana, kusaidiana na kuoneana huruma, ambapo waislamu wenye uwezo waliwasaidia watu wenye mahitaji, wakiwemo mayatima, wajane, wazee pamoja na mafukara, hivyo akataka jambo hilo kuendelezwa,

Alhadj Rais Dk.Mwinyi, alisema kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan ni msimu maalum wa mafunzo juu ya mambo ya msingi , ikiwa ni hatua ya Mwenyezi Mungu ya kuwaleta waja wake duniani kwa lengo la kumuabudu peke yake bila kumshirikisha.

Alisema waislamu wana wajibu mubwa wa kuyaendeleza na kuyadumisha yale waliyojifunza ili waweze kufanikiwa katika maisha yao ya dunia na akhera.

Alisisitiza umuhimu wa kujikurubisha kwa Mola na kufanya ibada za sunna na fardhi , kama ilivyokuwa katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambapo waislamu waijitahidi kudumu katika tabia na mwenendo mwema.

Alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwapa neema waislamu na kuweza kusali sala ya Iddi katika Misikiti na Viwanja mbali mbali Unguja na Pemba, ambapo sala hiyo kitaifa ilisaliwa katika viwanja vya Maisara, hali ya kuwa nchi iko katika hali ya amani na utulivu.

Aidha, alitoa shukran kwa Masheikh na walimu kwa kazi kubwa ya kuendesha darsa misikitini, katika kumbi pamoja na kutumia vyombo vya habari kuwakumbusha waislamu wajibu wa kusoma Qur-an ili kuimarisha ibada zao.

“Nawashukuru kwa kuandaa mashindano katika maeneo ya kuhifadhi qur-an, yakiwemo mashindano ya kuhifadhi Qur-an ya Kimataifa yaliofanyika katika Uwanja wa Amani April 24, 2021 ambayo yalifanikiwa na kufana sana”, alisema.

Alhadj Dk. Mwinyi aliwashukuru wananchi na wageni ambao katika kipindi cha mwezi mtukufu hawakuwa katika funga, lakini walionyesha ushirikiano kwa ndugu zao waliokuwa kwenye swaumu.

Viongozi mbali mbali wa Kitaifa, wakiwemo Marais wastaafu, wake wa Viongozi wakuu, viongozi wa serikali, vyama vya Siasa, viongozi wa Dini, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na wananchi walihudhuria hafla hiyo.

Mapema, Alhadj Dk. Mwinyi aliungana na mamia ya waumini wa Dini ya Kiislamu katika sala ya Idd el Fitri iliyosaliwa katika viwanja vya Maisara, jijini hapa.

Sala hiyo iliongozwa na Sheikh Rashid Said Daud, wakati ambapo katika khotuba iliosomwa na Sheikh Abdurahim Said Abdalla, alisisitiza umuhimu wa waislamu kuendelea kudumu katika kufanya mambo mema na kuepukana na maasi.

Katika hafla hiyo, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilipiga mizinga kuashiria ibada hiyo.

Katika hatua nyengine, Rais Alhadj Dk. Mwinyi alipata fursa ya kusalimiana na Masheikh kutoka maeneo mbali mbali Unguja na Pemba waliofika Ikulu Jijini hapa, ambapo pamoja na kuwapa zawadi ya sikukuu ya Eid el Fitri, aliwatakia kheri ya sikukuu hiyo.

Aidha, Alhadj Dk. Mwinyi aliwatunuku zawadi wananchi na watoto waliofika Ikulu Zanzibar kupokea mkono wa Idd el Fitri.

Wakati huo huo; Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhadj Dk. Hussein Mwinyi alirudia kauli yake na kusisitiza kuwa Serikali itafanya kila linalowezekana ili kuhakikisha Mahujaji wa Zanzibar wanakamilisha masharti yatakayowekwa, ili waweze kushiriki ipasavyo Ibada ya Hijja, nchini Saud Arabia baadae mwaka huu.

Akizungumza na waumini wa Dini ya Kiislamu katika sala ya ijumaa Msikiti wa Ijumaa Malindi; Mkoa wa Mjini Magharibi, Alhadj Dk. Mwinyi alisema Serikali itafanya juu chini kuwawezesha Mahujaji kutimiza masharti ya ushiriki wa Ibada hiyo, baada ya Serikali ya Saud Arabia kuondoa zuio lilitokana na Ugonjwa wa Covid-19.

Alisema taarifa za awali zilizopokelewa kutoka nchi hiyo; zimebainisha miongoni mwa masharti yanayohitajika kufanikisha ushiriki huo ni pamoja na waumini kuwa na umri usiozidi miaka 60.

Alisema Mahujaji wote watakaoshiriki Ibada hiyo mwaka huu ni lazima wawe wamepata chanjo ya Ugonjwa wa Covid – 19.

Alhadj Dk. Mwinyi, alitumia fursa hiyo kuwataka waumini wote wenye nia ya kushiriki Ibada hiyo kujiandaa.

Aidha, aliwakumbusha waislamu umuhimu wa siku ya Idd el Fitri ya kuwatembelea ndugu na jamaa na kutakiana kheri, sambamba na kuushukuru Uongozi wa Msikiti huo kwa kumpa fursa ya kuzungumza na waumini.

Alhadj Dk. Mwinyi alipata fursa ya kuzuru makaburi ya Masheikh mbali mbali maarufu waliozikwa katika eneo la msikiti huo. 

Nae, Khatibu katika sala hiyo Sheik Ameir Muhidin, amewataka waumini wa dini hiyo kufuatilia nyendo za watoto wao wakati huu Waislamu wakisherehekea sikukuu ya Eid el Fitri, kw akigezo kuwa hujitokeza matukio mbali mbali yasio halali.

Aliwataka kuwa wachunga wa watoto wao ili kupata radhi za Mwenyezi Mungu.