Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewasisitiza Waumini wa Dini ya Kiislamu na Wananchi kwa ujumla kuendelea kuiombea Nchi Amani.Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 21 Novemba 2025 alipojumuika na Waumini wa Dini ya Kiislamu katika Sala ya Ijumaa iliyosaliwa Masjid Rashidin, Dole Sokoni, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Ameeleza kuwa ni jukumu la kila mmoja kutumia nafasi yake kuhimizana na kukumbushana umuhimu wa Amani nchini, pamoja na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya Amani iliyokuwepo kabla ya Uchaguzi, wakati wa Uchaguzi na baada ya Uchaguzi. Alhaj Dkt. Mwinyi amefahamisha kuwa kuwepo kwa Amani kunaiwezesha Nchi kutekeleza mipango ya Maendeleo katika nyanja mbalimbali, na kuunga mkono hatua ya kutangaza siku ya Jumatatu tarehe 24 Novemba 2025 kuwa siku maalum kwa Waumini kufunga kwa ajili ya kuiombea Nchi Amani.
Alhaj Dkt. Mwinyi amesema kuwa madhara ya ukosefu wa Amani ni makubwa, ikiwemo kupungua kwa upatikanaji wa bidhaa muhimu za chakula, kupanda kwa bei za bidhaa, na kuwepo kwa misukosuko ya kijamii.Amesisitiza umuhimu wa kuiombea Nchi Amani ili kuepusha mitafaruku ya aina hiyo.
Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi amewaomba Waumini wa Dini ya Kiislamu kuwaombea dua Viongozi Wakuu wa Serikali ili waweze kutekeleza majukumu na ahadi zao kwa mafanikio, kwani wamekabidhiwa dhamana kubwa ya kuwatumikia Wananchi.
