RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, AlhajDk. Hussein Ali Mwinyi ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Kusini Unguja kwa uratibu mzuri wa hafla ya futari.Alhaj Dk. Mwinyi ameusifu uongozi huo kwa kugusa makundi yote ya jamii yenye uhitaji.

Pia Alhaj Dk. Mwinyi aliwashukuru wananchi wa Mkoa huo kwa kukubali kwao kujumuika pamoja nae kwenye futari ya pamoja aliyowaandalia, ikiwa ni kawaida yake aliyojipangia kila ifikapo mwezi mtukufu wa Ramadhan kufutari na wananchi katika kutekeleza ibada ya mfungo huo ambapo pia ameeleza kuwa ameirithi kwa viongozi waliomtangulia.

“Nakushukuruni nyote kwa muitikio wenu kuja kuungana nami kwenye hafla hii…..”

“......nimemuomba Mkuu wa Mkoa huu awawakilishe wananchi kwa makundi na amefanya hivyo, basi nimefurahi hata nyinyi mliowakilisha wenzenu tumefurahi pamoja, Mwenyezi Mungu akulipeni kila la kheri” alisifu Dk. Mwinyi.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud alitoa shukrani kwa Alhaj Dk. Mwinyi kwa niaba ya wananchi wa Mkoa huo hasa kwa kufutarishwa pamoja na kupokea sadaka za futari kwa wananchi wenye kipato cha chini zaidi kwa Wilaya zote mbili za Mkoa huo.

Hafla hiyo ya kuwafutarisha wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja, iliandaliwa na Alhaj Dk. Mwinyi ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, Serikali, vyama vya siasa na wananchi wa makundi yote wakiwemo wazee, wajane, watu wenye ulemavu, watoto, yatima, wananchi wenye uhitaji, maimamu wa misikiti ya Wilaya zote za Kati na Kusini Unguja, walimu wa madrasa, wawakilishi wa asasi za kiraia na wawakilishi wa bodaboda.

Alhaj Dk. Mwinyi kila ifikapo mwezi Mtukufu wa Ramadhan hujumuika pamoja na wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba kujenga umoja, ushirikiano, mshikamano, upendo na kuimarisha amani baina ya viongozi na wananchi.