Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametangaza kuwa atalivunja rasmi Baraza la Kumi la Wawakilishi ifikapo tarehe 13 Agosti 2025.Akizungumza katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kilichofanyika leo, tarehe 23 Juni 2025, Chukwani, Mkoa wa Mjini Magharibi, Dkt. Mwinyi amesema kuwa hatua hiyo ni kwa mujibu wa Kifungu cha 92 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Katika hotuba yake, Rais Dkt. Mwinyi ameelezea kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake ni pamoja na kuimarika kwa uchumi, kuendelezwa kwa amani, na mafanikio ya kuwaleta wananchi pamoja bila kujali rangi, asili, jinsia, dini au itikadi za kisiasa. Pia amesisitiza kuendelea kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Kuhusiana na Muungano, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa mafanikio yamepatikana katika kuimarisha Muungano wa Tanzania kisiasa, kiuchumi na kijamii, tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa kushughulikia hoja za Muungano mwaka 2006, ambapo hoja 26 zimejadiliwa na 22 kupatiwa ufumbuzi.
Akihitimisha hotuba yake, Rais Dkt. Mwinyi amewasisitiza wananchi kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura na kushiriki uchaguzi kwa kudumisha amani kabla, wakati, na baada ya uchaguzi. Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa, asasi za kiraia na viongozi wa dini kutekeleza wajibu wao wa kikatiba katika kipindi hiki muhimu.
Amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) kupitia Tume za Uchaguzi za ZEC na NEC, inaendelea na maandalizi ya uchaguzi kwa misingi ya haki na sheria.
Mapema, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mhe. Zubeir Ali Maulid, alitangaza rasmi kumalizika kwa maisha ya Baraza la Kumi la Wawakilishi kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, na kumshukuru Rais wa Zanzibar kwa ushirikiano wake pamoja na kuwashukuru wajumbe wa Baraza kwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.