Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuimarisha utumishi wa umma kwa kulinda misingi ya uwajibikaji, kukuza matumizi ya teknolojia ya kisasa na kuhimiza ubunifu unaolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 17 Juni 2025 alipozindua rasmi Kongamano la Kwanza la Kitaaluma la Utumishi wa Umma, lililoandaliwa kwa ushirikiano wa Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar (IPA) na Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC), lililofanyika hoteli ya Verde, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha Rais Dkt. Mwinyi amesema utumishi wa umma ni uti wa mgongo wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa, hivyo mafanikio ya taifa lolote yanategemea kwa kiasi kikubwa ubora wa huduma zinazotolewa na sekta hiyo. Amepongeza kaulimbiu ya kongamano hilo isemayo “Mchango wa Uongozi, Teknolojia na Ubunifu katika Kufikia Tanzania Tuitakayo”, akieleza kuwa inaweka msingi thabiti wa mjadala wa mageuzi chanya katika taasisi za umma.
Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inachukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa mifumo ya kidijitali inatumika kuongeza uwazi, kuondoa urasimu na kufikisha huduma kwa wananchi kwa njia rahisi na kwa wakati. Amesema TEHAMA ni nyenzo muhimu ya mageuzi hivyo ni lazima watumishi wa umma wajengewe uwezo wa kufikiri nje ya mipaka ya kawaida.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Mwinyi amewataka Watumishi wa Umma kuendelea kujituma kwa dhati, kuwa na uadilifu usiotetereka na kuwahudumia wananchi kwa moyo wa kizalendo.