Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa wakati umefika kwa Tanzania, ikiwemo Zanzibar, kuimarisha ushirikiano katika kutekeleza diplomasia ya kiuchumi na Zimbabwe.Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na Balozi wa Zimbabwe nchini Tanzania, Hellen Bawange Dingani, aliyefika Ikulu Zanzibar kujitambulisha rasmi.

Rais Dkt. Mwinyi amesema uhusiano wa muda mrefu baina ya nchi hizo mbili umejengwa vema kisiasa tangu enzi za harakati za kupigania uhuru, hivyo huu ni wakati muafaka kuelekeza nguvu katika diplomasia ya uchumi kwa manufaa ya pande zote mbili.Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Zanzibar ina fursa nyingi na maeneo mbalimbali ya ushirikiano wa kiuchumi ambayo yanaweza kushirikishwa na Zimbabwe, hususan katika sekta za biashara, utalii, na uwekezaji.

Aidha, Dkt. Mwinyi ametoa rai ya kuandaliwa kongamano maalum kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na Zimbabwe ambalo litalenga kubainisha fursa na maeneo mahususi ya ushirikiano wa kibiashara.Ameongeza kuwa licha ya Zanzibar kupokea watalii kutoka Zimbabwe, bado ipo fursa pana ya kuongeza idadi hiyo kwa kuimarisha ushirikiano katika kukuza sekta ya utalii kati ya nchi hizo.

Kwa upande wake, Balozi Hellen Bawange amesema Zimbabwe inaendelea kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na Tanzania katika harakati za ukombozi wa bara la Afrika, na kwamba nchi hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania. Balozi Hellen pia amesisitiza umuhimu wa vyama vya CCM na ZANU-PF kuendeleza ushirikiano wa karibu zaidi, hasa wakati huu ambapo vuguvugu la harakati hasi dhidi ya vyama vya kihistoria barani Afrika linazidi kushika kasi.

Mwisho, Balozi Hellen amewasilisha salamu rasmi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Dkt. Emmerson Dambudzo Mnangagwa, kwa Rais Dkt. Mwinyi.