Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameihimiza Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kuendelea kuwekeza katika teknolojia, usalama wa mifumo ya kifedha, ubunifu wa bidhaa na huduma, pamoja na matumizi ya akili mnemba (AI), ili kuongeza ufanisi na ushindani katika utoaji wa huduma.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 30 Juni 2026, katika Maadhimisho ya Miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), yaliyofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar Airport, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema maendeleo ya teknolojia yanaendelea kuibadilisha dunia kwa kasi, hivyo taasisi za kifedha zinapaswa kwenda sambamba na mabadiliko hayo ili kukidhi mahitaji ya wateja wa kizazi cha sasa na kijacho.

Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza PBZ kwa juhudi zake za kuendeleza huduma za kidijitali, kutumia teknolojia za kisasa na kuimarisha mifumo inayorahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi.

Dkt. Mwinyi ameitaka PBZ, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, kuongeza juhudi za kuimarisha huduma zake ili ipande kutoka nafasi ya sita iliyopo sasa na kuwa benki bora zaidi nchini Tanzania.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameihimiza PBZ kuendelea kuzingatia mambo muhimu yafuatayo:
1. Kuimarisha mtaji wa benki hiyo.
2. Kuongeza ubunifu wa bidhaa na huduma za kifedha.
3. Kuendelea kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi.
4. Kukuza uwekezaji katika rasilimali watu.
5. Kuimarisha utawala bora na usimamizi wa vihatarishi.
6. Kuendelea kuwa mshirika wa Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Rais Dkt. Mwinyi amewapongeza viongozi wote waliowahi kuitumikia PBZ tangu kuanzishwa kwake mwaka 1966, wafanyakazi kwa kujituma, pamoja na wateja kwa kuendelea kuiamini benki hiyo.

Amesema katika kipindi cha miaka 60, PBZ imethibitisha kuwa taasisi ya kifedha inayoheshimika ndani na nje ya nchi, huku ikiendelea kutekeleza malengo ya kuanzishwa kwake, kushirikiana na Serikali katika miradi ya maendeleo na kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kutekeleza Dira ya Maendeleo inayolenga kujenga uchumi wa kisasa, jumuishi na wenye ushindani, huku mafanikio makubwa yakipatikana katika sekta za miundombinu, afya, elimu, uwekezaji, utalii, biashara, uchumi wa buluu na mageuzi ya huduma za Serikali kwa kutumia teknolojia.

Rais Dkt. Mwinyi amesema gawio la shilingi bilioni 15.3 lililotolewa na PBZ kwa Serikali ni ushahidi wa kuimarika kwa hali ya kifedha ya benki hiyo, usimamizi mzuri wa rasilimali zake na mchango wake katika kugharamia miradi ya maendeleo na huduma za kijamii.

Akihitimisha hotuba yake, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza matarajio yake ya kuiona PBZ katika miaka 30 ijayo ikiwa Benki ya Watu na Chaguo la Watu, iliyo kubwa na imara zaidi, yenye mtandao mpana wa huduma, inayotambulika kwa ubora, ubunifu na ujumuishaji wa kifedha, pamoja na kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya wananchi na uchumi