RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka wahitimu wa vyuo vikuu nchini kujikita na tafiti zitakazotoa ufumbuzi wa matatizo yaliyomo kwenye jamii.Aidha, alivitaka vyuo vikuu kuongeza fani kwa mujibu wa mahitaji ya wakati uliopo na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia duniani ili kuleta mabadiliko nchini.

Dkt. Mwinyi alitoka kauli hizo kwenye Mahafali ya 22 ya Chuo Kikuu cha Abdulrahman Al- Sumait, Chukwani Wilaya ya Magharibi B, Unguja.Aliwataka wahitimu hao kutumia tafiti zao kwa lengo la kutatua changamoto zilizomo kwenye jamii badala kuziweka kwenye makbtaba na kuzifungia.Rais Dk. Mwinyi, alizishauri Wizara na Idara za Serikali kushirikiana na vyuo vikuu kufanya tafiti zenye kuchochea maendeleo kwenye nyanja zote za jamii na uchumii, tehama na mawasiliano ili kutela mabadiliko yenye tija.

“Nazishauri Wizara na Idara za Serikali kushirikiana na wataalamu wa vyuo vikuu, kufanya tafiti zitakazosaidia kuchochea maendeleo katika nyanja za kijamii, uchumi na teknolojia ya habari na mawasiliano ili kuendelea kusonga mbele” Alishauri Dk. Mwinyi.Katika hatua nyengine Rais Dk. Mwinyi, aliwasihi wahitimu watakao bahatika kuajiriwa ama kujiajiri baada ya kuhitimu mafunzo yao, wakafanye kazi kwa uadilifu, kujituma na kuchunga maadili katika jamii zao, kwa kuleta mabadiliko kwenye utendaji wao.

Aidha, aliwataka wakawe wabunifu wa kuzitafuta fursa na kuzitumia ili wajiendeleze kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu kwa lengo la kujiimarisha kitaaluma.
Hata hivyo, aliwaasa wanafunzi wanaoendelea na masomo chuoni hapo kuendelea kudumisha nidhamu na kufuata mazuri ya watangulizi wao na kufuata maadili mema ya kutafuta elimu ili wapate ufaulu mzuri.

Akizungumza kwenye mahafali hayo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhamed Mussa alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inania ya kutanua wigo kwenye skuli za umma kwa kuweka kipaumbele kwenye mafunzo ya Amali ya ufundi ili kuwapa uwezo wanafunzi wanaomaliza masomo yao wajiajiri.Alisema Sera ya elimu inawataka wanafunzi watakapomaliza masomo yao yalazima kwa ngazi ya sekondari, kuwe na sehemu ya kupata kujiendeleza kwa stadi za ufundi na vitendo.

“Lazima tuwe na taasisi, tuwe na vyuo vyenye kutoa fani tofauti ambazo wanafunzi watajiajiri baada ya masomo yao” Alishauri Waziri Lela.Aliongeza kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Sumait kumekua msaada mkubwa katika kuendeleza juhudi za Serikali.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Msafiri Mshewa aliwataka wahitimu hao wakasaidie kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii zao kwa kutumia vizuri ujuzi wa taaluma zao kuongeza tija. Aidha, aliwataka wawe mabalozi wazuri wa kuzikimbilia fursa kwa kuzifanyia kazi zenye tija.“Ni matumaini yetu elimu mliyoipata itawanufaisha nyinyi, jamii na Watanzania kwa ujumla, kila mmoja wenu anawajibu na nafasi ya kuchangia maendeleo kwa kuangalia eneo la taaluma yake litakavyosaidia kuleta mageuzi ya maendeleo kwa kuajiriwa ama kujiajiri wenyewe” Aliwaasa wahitimu hao.

Chuo cha Abdulrahman Al Sumait chini ya uongozi wa Mkuu wake, Dk. Aman Abeid Karume, Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya sita, kimeanzishwa mwaka 1998. Jumla ya wahitimu 310 wakiwemo wanawake 183 na wanaume 127 walikamilisha masomo kwenye mahfali ya 22 ya chuo hicho, wahitimu 18 kati yao walitunukiwa shahada ya udhamili, 241 shahada ya kwanza na 51 walitunukiwa stashahada na astashahada.