Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Serikali ya Awamu ya Nane katika nyanja mbalimbali yanatokana na mchango mkubwa wa Mhimili wa Baraza la Wawakilishi.Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika hafla ya kuwapongeza na kuwaaga Wajumbe wa Baraza la Kumi la Wawakilishi, iliyofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege, Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe 23 Juni 2025.
Aidha Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa anauthamini mchango mkubwa uliotolewa na Mhimili huo wa Baraza la Wawakilishi katika kujenga nchi.Amefahamisha kuwa utekelezaji bora wa kazi za mihimili ya nchi ambayo ni Mahakama, Serikali na Baraza la Wawakilishi umekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha majukumu ya kuwahudumia wananchi.
Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amefafanua kuwa umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na Baraza la Wawakilishi unaongeza uwajibikaji kwa kuwepo kwa usimamizi na ufuatiliaji mzuri wa Serikalini.Rais Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwasisitiza Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu kwa kupiga kura, na kila mwenye sifa na haki ya kushiriki uchaguzi kufanya hivyo.
Rais Dkt. Mwinyi amewaaga na kuwatakia kila la heri Wajumbe wa Baraza la Kumi la Wawakilishi, ambao wameagwa rasmi baada ya Rais kutangaza kuwa atalivunja Baraza hilo ifikapo tarehe 13 Agosti 2025, mara baada ya kumaliza kipindi cha miaka mitano kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.Baraza la Wawakilishi limemtunuku Rais Dkt. Mwinyi Tuzo Maalum kwa kuthamini na kutambua mchango wake mkubwa kwa Baraza hilo, sambamba na uongozi wake unaoleta mageuzi katika sekta mbalimbali za maendeleo.