Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewaapisha Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu aliowateua hivi karibuni, na kuwaagiza waache kukaa Maofisini bali washuke chini kuwatumikia Wananchi. Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 22 Novemba 2025 katika hafla ya kuwaapisha Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, hafla iliyofanyika katika Viwanja vya Ikulu, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Rais Dkt. Mwinyi amewasisitiza Watendaji hao Wakuu kuyazingatia mambo matano muhimu katika utekelezaji wa majukumu yao ambayo ni: Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2025 hadi 2030 kwa kuandaa Mpango Kazi wa utekelezaji wa yaliyomo katika Ilani hiyo, kusoma na kuifahamu Hotuba ya Ufunguzi wa Baraza la Wawakilishi, kuwa na Mpango Kazi wa utekelezaji wa Ahadi za Kampeni, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar, pamoja na Mpango Mkuu wa Maendeleo Zanzibar.
Rais Dkt. Mwinyi amewaeleza Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu kuwa mambo hayo matano ndiyo nyenzo na dira muhimu za utekelezaji wa majukumu yao. Aidha Rais Dkt. Mwinyi amewaagiza kuzingatia mambo mawili muhimu katika maeneo yao ya kazi ambayo ni Usimamizi Bora wa Utawala na Fedha, na kuwataka waongoze Taasisi zao vizuri kwa kuondoa makundi, kwa dhamira ya kuwatumikia vema Wananchi.
Akizungumzia masuala ya Fedha, amewasisitiza kuhakikisha matumizi mazuri ya Fedha za Umma kwa kuondoa matumizi yasiyo na tija kwa Nchi, sambamba na kuhakikisha ukusanyaji wa kutosha wa Mapato ya Serikali. Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia Watendaji hao Wakuu kuwa endapo watajipanga vema na kutekeleza kwa umakini miongozo hiyo mitano, Serikali itaweza kutekeleza Miradi ya Maendeleo na matarajio ya Wananchi kwa ufanisi mkubwa.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Nchi inahitaji kasi mpya ya utekelezaji ili kuleta Maendeleo, hivyo kila mmoja anapaswa kuendana na kasi na dhamira ya Serikali ya kuleta huduma bora kwa Wananchi. Rais Dkt. Mwinyi amesema Afisi ya Rais iko wazi kwa ushirikiano, maoni na ushauri ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Watendaji hao Wakuu.
