Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa mageuzi ya uchumi na fedha yaliyotekelezwa na Serikali yamekuwa msingi muhimu wa kuijenga Zanzibar inayowashirikisha wananchi wote katika ujenzi wa taifa.

Akizungumza katika hafla maalum ya kumpongeza kwa mageuzi ya uchumi na fedha, pamoja na utoaji wa gawio kwa wawekezaji wa Zanzibar Sukuk na uzinduzi wa Skimu ya Hifadhi ya Jamii ya Kiislamu, hafla iliyofanyika katika Viwanja vya Ikulu Zanzibar leo tarehe 20 Oktoba 2025, Rais Dkt. Mwinyi alisema Serikali imepiga hatua kubwa katika kuimarisha uchumi wa nchi.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali imefanikiwa kutokana na sera madhubuti, mifumo ya kisasa na usimamizi bora wa fedha za umma hali iliyosababisha uchumi kukua kwa asilimia 7.2, ongezeko la uwekezaji wa ndani na nje ya nchi, udhibiti wa mfumuko wa bei kwa tarakimu moja, na ongezeko la mapato kwa asilimia 278 ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita. Aidha, sekta za huduma kama utalii, kilimo na uvuvi zimeendelea kuimarika kwa kasi.

Rais Dkt. Mwinyi alibainisha kuwa mageuzi hayo yametekelezwa chini ya misingi ya uwazi, uwajibikaji na matumizi ya teknolojia za kisasa, akisisitiza kwamba hatua ya kutoa gawio la kwanza kwa wawekezaji wa Zanzibar Sukuk tangu kuanzishwa kwake mwaka 2024 ni ishara ya dhamira ya Serikali katika kusimamia vyema dhamana zake.

Kupitia mpango wa Sukuk, Serikali imefanikiwa kugharamia miradi mbalimbali ya kimkakati, kuimarisha imani kwa wawekezaji, na kufungua milango kwa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi alisema hatua hiyo inaweka Zanzibar katika historia mpya ya kifedha inayozingatia misingi ya sheria za Kiislamu. Aliongeza kuwa mafanikio ya uchumi shirikishi hayawezi kufikiwa bila mfumo imara wa bima, hivyo Serikali kupitia Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC) imeanzisha mfumo wa bima ya Kiislamu utakaotoa huduma zinazofuata sheria hizo.
Katika kuhitimisha hotuba yake, Rais Dkt. Mwinyi alisema Serikali imefanya mageuzi makubwa katika mifumo ya hifadhi ya jamii, kwa kuimarisha utendaji wa mifuko ya jamii ili kuhakikisha wastaafu wanalipwa kwa wakati, michango inasimamiwa kwa uwazi, na faida zinawanufaisha wanachama wote.

Amesisitiza kuwa kupitia mifumo ya kidijitali, Serikali itahakikisha kila mfanyakazi wa umma na sekta binafsi anasajiliwa na kulindwa dhidi ya changamoto za kiuchumi, uzee, maradhi na ajali — hatua ambayo alisema itaiimarisha Zanzibar yenye haki, usawa na ustawi wa jamii.

Katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Fedha na Mipango, Mhe. Saada Mkuya Salum, alimkabidhi Rais Dkt. Mwinyi tuzo maalum kutambua mchango wake mkubwa katika mageuzi ya uchumi na sekta ya fedha nchini.