Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameishukuru Serikali ya Saudi Arabia kwa kuendelea kudumisha na kuimarisha ushirikiano wa kindugu na wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili, akibainisha kuwa ushirikiano huo umejengwa juu ya misingi ya kuheshimiana, mshikamano na maslahi ya pamoja.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 19 Januari 2026, Ikulu Zanzibar, alipokutana na Waziri wa Hijja na Umrah wa Saudi Arabia, Mhe. Tawfiq bin Fawzan Al-Rabiah, aliyefika kuonana naye akiambatana na Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Mhe. Yahya bin Ahmed Okeish.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi ameomba Serikali ya Saudi Arabia kuendelea kuunga mkono Mfuko wa Hijja wa Zanzibar (Zanzibar Haj Fund) ili kuimarisha maandalizi na mazingira ya mahujaji wa Zanzibar, pamoja na kuendeleza ushirikiano katika elimu ya Kiislamu kwa kuongeza fursa za masomo kwa wanafunzi wa Zanzibar nchini Saudi Arabia.

Aidha, ameishauri Saudi Arabia kuangalia uwezekano wa kuongeza safari za ndege kati ya Saudi Arabia na Zanzibar, hususan kipindi cha Hijja.

Kwa upande wake, Mhe. Al-Rabiah ameipongeza Zanzibar kwa mageuzi ya miundombinu, ikiwemo viwanja vya ndege na barabara, akibainisha kuwa hatua hiyo imechochea ongezeko la watalii na ukuaji wa uchumi, na ameihakikishia Zanzibar kuendelea kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali