Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameipongeza Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Dodoma kwa mageuzi na mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi.R ais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 4 Machi 2026, alipokutana na Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Prof. Abel Makubi, akiambatana na ujumbe wake, waliofika Ikulu, Zanzibar.
Rais Dkt. Mwinyi amesifu hatua kubwa ya utoaji wa huduma za kibingwa, ikiwemo matibabu ya figo, moyo na ubongo kufanyika nchini, hatua aliyoielezea kuwa imeipunguzia Serikali na wananchi gharama za kuwapeleka wagonjwa kutibiwa nje ya nchi. Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameuishauri uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa kuendeleza utaratibu wa matibabu ya nje kwa kuwafikia wananchi katika maeneo yao kupitia mpango wa outreach programme, kwani unasaidia kuwatibu watu wengi zaidi.
Rais Dkt. Mwinyi ameahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Wizara ya Afya Zanzibar, itaendeleza ushirikiano na Hospitali ya Benjamin Mkapa na kutafuta njia bora zaidi za kufanya kazi kwa pamoja. Pia ameipongeza hospitali hiyo kwa kuendeleza mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji kupitia taasisi za ndani na wadau kutoka nje ya nchi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi, ameeleza kuwa hospitali hiyo imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka kumi tangu kuanzishwa kwake kwa kutoa huduma za matibabu bobezi na kibingwa zaidi ya 20, ikiwemo upandikizaji wa figo, upasuaji wa ubongo na matibabu ya moyo, hali iliyochangiwa na jitihada za Serikali kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya afya.
.jpeg)